Connect with us

General News

Raila atuliza vita vya ndani katika Azimio – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Raila atuliza vita vya ndani katika Azimio – Taifa Leo

Raila atuliza vita vya ndani katika Azimio

VALENTINE OBARA NA STEPHEN ODUOR

MGOMBEA urais kupitia Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga, ameanza kutuliza joto la ushindani wa vyama tanzu ndani ya muungano huo.

Kwa wiki kadha sasa, suala la kutengea baadhi ya vyama maeneo katika uchaguzi wa Agosti 9 limekuwa likiibua kiwewe baina ya wanasiasa, wakihofia kuwa watalazimika kuachia wenzao nafasi ili Azimio iwe na mgombeaji mmoja.

Mbali na hayo, wito wa Bw Odinga kwa wafuasi, hasa katika ngome zake za kisiasa, kupigia kura wanachama wake pekee pia ulikera wagombea wa vyama tanzu, waliolalama kwamba hilo si haki sababu wao wanampigia debe kwa wadhifa wa urais ilhali anawakata miguu mashinani.

Akizungumza Jumatano katika Kaunti ya Tana River, Bw Odinga alihimiza wafuasi wa muungano huo kutochukulia ushindani wa wagombea katika vyama tanzu vya Azimio, kama uadui.Kulingana naye, jambo muhimu ambalo wafuasi wa Azimio wanastahili kutilia maanani ni jinsi ya kuzuia Muungano wa Kenya Kwanza kupata viti vingi vya kisiasa kwenye uchaguzi ujao.

“Mimi ndiye mgombeaji wa urais wa Azimio, hakuna mwingine. Jeshi letu liko upande huu, wale wako upande ule mwingine. Tuwe timu moja kama wawaniaji wa Azimio. Ushindani wetu uwe kama ule wa kifamilia. Maadui tunaopigana nao ni Kenya Kwanza,” alisisitiza Bw Odinga.

Waziri huyo mkuu wa zamani, ambaye pia ni kinara wa chama cha ODM, aliwasili Pwani usiku wa kuamkia jana mjini Malindi, Kaunti ya Kilifi.

Alielekea Tana River asubuhi ambapo baraza la wazee lilimtawadha Gavana Dhadho Godhana kutetea kiti chake na pia kuwa msemaji wa jamii ya Wapokomo kisiasa.

Ushindani ndani ya Azimio inahofiwa utasababisha migogoro ambayo itaathiri ufuasi wa Bw Odinga, na kumpa mpinzani wake wa karibu Naibu Rais William Ruto mteremko uchaguzini.

Vile vile, wadadisi wameonya kuwa wito wa kutaka wapigakura wachague wagombea wa ODM pekee katika nyadhifa zote za ushindani, unaweza kufanya wawaniaji wa vyama tanzu kujiepusha kumpigia debe Bw Odinga kwa urais, ilhali wengi wao wana ufuasi unaoweza kumuongezea kura katika kapu lake.

Kiongozi huyo wa ODM pia alitaka kuwe na maridhiano kati ya wawaniaji walioshinda kura ya mchujo na wenzao waliobwagwa, akihofia uwezekano wa wale waliobwagwa kuhamia mrengo wa upinzani.

Baadhi ya walioshindwa tayari walielekea Kenya Kwanza inayoongozwa na Naibu Rais Dkt Ruto.

Mbali na hayo, alisisitiza kuwa akishinda urais mojawapo ya ajenda za kwanza ni kurudisha mchakato wa marekebisho ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI), ili kuongeza mgao wa fedha kwa kaunti.

Wakati huo huo, alisema manifesto ya Azimio iko tayari.

“Manifesto yetu itazinduliwa Nairobi wiki ijayo, na itawapa mwongozo wa sera mtakayotumia kwa kampeni,” akasema.

Alikuwa ameandamana na viongozi wengine wa Azimio akiwemo Kiongozi wa Narc Kenya, Bi Martha Karua, Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, Mbunge Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Murang’a, Bi Sabina Chege, Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed, miongoni mwa wengine.

Bw Joho alimkashifu Dkt Ruto aliyesema akishika hatamu ya uongozi atabadili sera na sheria za uchukuzi wa mizigo kwa SGR kwa manufaa ya Mombasa.

Kulingana naye, Dkt Ruto alikuwa mstari wa mbele kumkosoa na kumtusi miaka iliyopita wakati yeye alipojitokeza kutahadharisha serikali kuhusu mipango ambayo ilihamisha biashara za uchukuzi wa mizigo kutoka Mombasa, na kuathiri uchumi wa mji huo.