Connect with us

General News

Rais ajaye asiogope madeni – Uhuru – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Rais ajaye asiogope madeni – Uhuru – Taifa Leo

Rais ajaye asiogope madeni – Uhuru

NA LEONARD ONYANGO

RAIS Uhuru Kenyatta jana Jumatano alitoa wasia kwa mrithi wake atakayechukua hatamu ya uongozi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Rais Kenyatta kupitia hotuba yake kwa taifa, alimtaka mrithi wake kupambana na ufisadi, kutimua wanafiki na asikubali kufanya kazi na viongozi wanaopinga miradi ya serikali.

Rais Kenyatta alisema mrithi wake hatafanikiwa kustawisha nchi iwapo hatakabili ufisadi.

“Ni sharti upambane na ufisadi serikalini kwanza kabla ya kuandama wafisadi walio nje,” akasema Rais Kenyatta.

Alimtaka mrithi wake kutoogopa madeni na badala yake aendelee kukopa ughaibuni kwa ajili ya ustawi wa nchi.

“Zimwi la ufisadi likimalizwa, deni halitakuwa mzigo kwa wananchi bali kichocheo cha maendeleo,” akashauri.

Alisema kuwa kujaa kwa wanafiki ndani ya serikali yake kulikwamisha maendeleo katika muhula wake wa kwanza kati ya 2013 na 2017.

“Kutokana na kuwepo kwa wanafiki, nilijenga kilomita 3,000 za barabara za lami katika muhula wangu wa kwanza.

“Lakini katika muhula wa pili nilifanikiwa kujenga barabara za lami za kilomita 6,600,” akasema Rais Kenyatta.

Alisema kuwa kufanya kazi na viongozi waasi wanaopinga kila mradi wa serikali ni hatari kwa utendakazi wa serikali.

Kiongozi wa nchi alitumia hotuba yake ya Jumatano kuorodhesha mafanikio ya serikali yake ndani ya miaka 10 iliyopita.

Alisema kuwa serikali yake imefanikiwa kuinua mapato ya wakulima wa kahawa ambapo sasa wanauza mazao yao kwa kati ya Sh110 na 125 badala ya Sh60 kwa kilo.

“Mapato yanayotokana na chai yameongezeka kutoka Sh114 bilioni hadi Sh454 bilioni kwa mwaka,” akasema.

Rais Kenyatta alisema kuwa amewezesha uchumi wa Kenya kuwa nafasi ya sita kwa ukubwa barani Afrika kutoka nafasi ya tisa 12 miaka 10 iliyopita.

Rais aliorodhesha mabwawa aliyojenga ikiwemo, Thiba (Kirinyaga), Yamo (Samburu).

“Tunaendelea na ujenzi wa mabwawa ya Thwake (Kitui/Machakos/Makueni), Mwache (Pwani), Karimenu (Kiambu), Siyoi Muruny (Pokot Magharibi), Bute (Wajir) na Soin Koru Dam (Nyanza).

“Tunaendelea na ujenzi wa miradi 685 ya maji kote nchinina kufikia mwishoni mwa mwaka huu asilimia 80 ya Wakenya watakuwa na maji safi,” akasema.

Alisema kuwa serikali yake imefanikiwa kuongeza eneo lililo chini ya kilimo cha unyunyiziaji maji kutoka ekari 374,000 mnamo 2013 hadi 664,000 mwaka huu.

Kulingana na kiongozi huyo, serikali ya Jubilee ilifanikiwa kuongeza idadi ya Wakenya wanaotumia kadi ya Bima ya Afya (NHIF) kupata huduma za matibabu kutoka milioni 4.4 miaka tisa iliyopita hadi milioni 17.1.

“Tumejenga hispitali na vituo vya afya 1,912 kote nchini tangu Jubilee ilipochukua hatamu ya uongozi 2013.

“Vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU) vimeongezeka kutoka 108 mnamo 2013 hadi 651. Vitanda vya kulaza wagonjwa viliongezeka kutoka 56,069 hadi 82,291 ndani ya kipindi sawa,” akasema.

Alisema kuwa alifanikiwa kutoa jumla ya Sh2.44 trilioni kwa serikali za kaunti kuendeleza miradi ya maendeleo tangu 2013.

Diplomasia

Alijipiga kifua katika juhudi za serikali yake kuinua sifa ya Kenya katika ngazi ya kimataifa.

“Kenya iliongoza juhudi za kuingiza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Vilevile, Kenya imejipatia nafasi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kenya ni kinara katika masuala ya kidiplomasia barani Afrika,” akasema.

Elimu

Rais Kenyatta pia aliorodhesha mfumo mpya wa Elimu ya Umilisi na Utendaji (CBC), kuteua idadi kubwa ya wanawake katika serikali yake, upanzi wa miti na ujenzi wa idadi kubwa ya vyuo anuai na ufundi kuwa miongoni mwa mafanikio yake.

“Mfumo wa CBC umeonyesha mafanikio makubwa na hakuna kurudi nyuma,” akasema.