Connect with us

General News

Rais Bio asimulia jinsi Kenya ilivyosaidia Sierra Leone – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Rais Bio asimulia jinsi Kenya ilivyosaidia Sierra Leone – Taifa Leo

Rais Bio asimulia jinsi Kenya ilivyosaidia Sierra Leone

NA MARY WANGARI

SHEREHE za Sikukuu ya Madaraka zilihudhuriwa na viongozi na wajumbe mashuhuri wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio, aliyekuwa mgeni wa heshima.

Rais Bio akiandamana na mke wake Fatima Jabbe Bio aliwasili Kenya Jumamosi usiku, Mei 28, 2022, kwa ziara ya siku tano nchini ambayo kilele chake ni Maadhimisho ya 59 ya Sikukuu ya Madaraka yaliyofanyika Jumatano katika Bustani ya Uhuru.

Akihutubia maelfu ya Wakenya waliohudhuria sherehe hizo, Rais wa Sierra Leone alisema japo safari ya uhuru kwa Kenya na Sierra Leone imekuwa yenye pandashuka tele, mahusiano kati ya nchi hizo mbili yamekuwa imara na yatazidi kuimarika hata zaidi.

“Mahusiano yetu yanazidi kuimarika. Jumapili nilijiunga na KDF kusherehekea Wakenya Shujaa waliopigania kurejesha amani Sierra Leone. Ikiwa hii leo taifa letu ndilo la nne lenye amani zaidi Afrika, ni kwa sababu ya Kenya ilivyojitolea mhanga. Ahsante Kenya. Ebola ilipozuka, madaktari na wauguzi Wakenya walikuwa tayari kutusaidia. Tulipokumbwa na changamoto ya vifaa katika shughuli yetu ya kwanza ya sensa kidijitali, Rais Kenyatta alitunyoshea mkono wa ukarimu wa Wakenya,” alisema Rais Bio.

Alisema kuwa nchi hizo mbili zimezidi kushirikiana katika nyanja za kibiashara huku akimpongeza Rais Uhuru kwa kufanikisha maendeleo ya kiuchumi nchini.

“Kazi kubwa ya Rais Kenyatta nchini humu kuanzia umeme, bandari, barabara, reli, makazi, huduma ya afya, elimu, chakula usalama na kukuza uchumi wa Kenya kupitia biashara na uwekezaji imetuonyesha sisi kama Sierra Leone kuwa inawezekana. Tuko hapa pia kuimarisha mahusiano yetu na Kenya katika nyanja za mashirika ya kimataifa, amani na usalama, wanyamapori, ICT, elimu, biashara na uwekezaji,”alisema.

Huku akinukuu misemo miwili kutika jamii ya Agikuyu na Mende, Sierra Leone, Rais Bio alisisitiza umuhimu wa Kenya na Sierra Leone kuendelea kufanya kazi pamoja ili kukabiliana na changamoto mbalimbali na kwa manufaa ya nchi hizo mbili.