Rais Kenyatta aungana na waombolezaji kwa ibada ya kumuaga shujaa Kibaki
NA SAMMY WAWERU
IBADA spesheli ya kumuaga Rais mstaafu Mwai Kibaki inafanyika leo Ijumaa katika uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi.
Mzee Kibaki alifariki Ijumaa wiki jana, na Rais Uhuru Kenyatta ameungana na waombolezaji wengine kwa ibada hiyo inayohudhuriwa na baadhi ya marais Barani Afrika, na viongozi mashuhuri ndani na kutoka nje ya nchi.
Mwili wa hayati ulitolewa katika makafani ya Lee dakika chache baada ya saa mbili asubuhi, kuelekea Ikulu ya Rais kwa ibada fupi ya maombi iliyoongozwa na Rais Kenyatta.
Jeneza lenye mwili wa Rais Kibaki na ambalo limefungwa bendera ya Kenya, lilibebwa na gari maalum na la hadhi la kijeshi chini ya msafara wa ulinzi mkali wa vikosi vya pamoja vya majeshi ya Kenya, KDF.
Mwanawe marehemu, Jimmy Kibaki na baadhi ya wanafamilia waliusindikiza wakiwa kwenye gari jingine la kijeshi lililokuwa nyuma.
Rais Kibaki atazikwa kesho, nyumbani kwake Othaya, Nyeri.
Mizinga 19 itafyatuliwa na maafisa wa KDF, kama ishara ya heshima kwa kiongozi aliyewahi kuhudumu kama Amiri Jeshi Mkuu.
Hayati anakumbukwa kama Shujaa aliyekomboa uchumi wa Kenya alipokuwa madarakani kati ya 2003 na 2013.
Licha ya ghasia za uchaguzi mkuu 2007 kushuhudiwa akitetea kuhifadhi kiti chake, Mzee Kibaki anamiminiwa sifa chungu nzima kutokana na miradi ya maendeleo aliyotekeleza.
Machafuko hayo ya baada ya uchaguzi, yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 1, 300 na maelfu kufurushwa makwao.
Mzee Kibaki, alifariki akiwa na umri wa miaka 90.