Njaa: Rais mpya wa Somalia alilia msaada
NA ABDULKADIR KHALIF
MOGADISHU, SOMALIA
RAIS mpya wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud ametoa wito kwa raia kuchangia katika mpango wa kuwasaidia wenzao walioathiriwa na ukame nchini humo, hasa walioko katika kambi za wakimbizi wa ndani kwa ndani (IDPs).
“Ninawahimiza Wasomali wote popote walipo kujitokeza kuwafaa watu ambao wameathirika na ukame. Watoe chochote walichonacho kuwasaidia watu hawa,” akasema.
“Watoto wetu walio katika kambi mbalimbali wanahitaji misaada ya kimsingi kama vile chakula na elimu,” Rais Mohamud akaongeza.
Kiongozi huyo pia alitoa wito kwa washirika wa kimataifa kuchangia katika mpango wa kuwasaidia raia hao wanaokabiliwa na njaa, magonjwa miongoni mwa changamoto nyingine.
Rais Mohamud alisema hayo Jumatano alipotembelea kambi mbalimbali za IDPs ndani na viungani mwa mji wa Baidoa. Mji huo mkuu wa jimbo la South West uko umbali wa kilomita 240 kutoka jiji kuu la Mogadishu.
Kambi hizo zinahifadhi maelfu ya watu ambao walitoroka makwao kwa hofu ya kuvamiwa na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al Shabaab.
Hata hivyo, wengi wao ni wahanga wa ukame mkali unaokumba sehemu nyingi za taifa hilo la upembe wa Afrika. Wakimbizi hao walisema kuna uhaba wa chakula na maji katika sehemu nyingi za mashambani, hali ambayo iliwalazimu kusaka usaidizi.
Mohamud, ambaye alichaguliwa Mei 15, aliwasili mjini Baidoa mnamo Jumanne katika ziara yake katika majimbo yote nchini Somalia kujifahamisha hali ilivyo katika maeneo hayo.
Mnamo Jumanne, afisa mmoja mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) la kutoa msaada wa kibinadamu nchini Somalia, Adam Abdelmoul, alisema hatua ya haraka inafaa kuchukuliwa kudhibiti ukame ambao umeathiri jumla ya watu milioni 7.1 nchini humo.
Miongoni mwa waathiriwa hao ni watoto 370,000 ambao wanazongwa na utapiaji mlo.
UKAME
Mnamo Machi 2022 UN ilionya kwamba Upembe mwa Afrika unakabiliwa na hali mbaya ya ukame kuwahi kushuhudiwa eneo hilo tangu 1981.
Umoja huo ulisema kuwa uhaba wa msaada wa kifedha unaweka maisha ya mamilioni ya raia nchini Somalia katika hatari zaidi.
“Mapigano yanayoendelea yamefanya hali kuwa mbaya zaidi. Makali ya ukame huu pia yamevuruga maisha ya mamilioni ya wakazi,” akasema Abdelmoul.
UN na mashirika yake iliomba msaada wa fedha kufadhili mipango ya usambazaji wa chakula cha msaada na mahitaji mengineyo.
Kulingana na Afisi ya Umoja wa Mataifa ya Kushirikisha Shughuli za Utoaji Misaada ya Kibinadamu (OCHA), Somalia ni mojawapo ya mataifa ya Upembe mwa Afrika ambayo imeathirika vibaya na ukame.