Connect with us

General News

Rais na naibu wake wamemkosea heshima Mzee Kibaki – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Rais na naibu wake wamemkosea heshima Mzee Kibaki – Taifa Leo

WANDERI KAMAU: Rais na naibu wake wamemkosea heshima Mzee Kibaki

NA WANDERI KAMAU

KATIKA tamaduni za Kiafrika, kuna muda ambao hutengwa ili kuipa jamii muda wa kutosha kumwomboleza aliyefariki.

Katika baadhi ya jamii, maombolezo huendelea hata kwa mwezi mmoja kulingana na umuhimu na mchango wa mwendazake.

Katika jamii nyingine, maombolezo huhusisha wanajamii kuepuka kutenda maovu kwa njia zozote zile kwa muda fulani, kama heshima kwa yule aliyefariki.

Vivyo hivyo, jambo kuu ni kuhakikisha kuwa aliyefariki ameagwa kwa njia ya amani na heshima.

Hapa nchini, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto ndio huonekana kama “wazazi” wa Wakenya, kutokana na majukumu muhimu ya uongozi wanayotekeleza.

Katika taswira ya kifamilia, wao ndio “mama” na “baba”, huku Wakenya wakiwa “watoto” wao.

Hivyo, wao ndio wanaotazamwa kwa kila hali—kuhusu matamshi wanayotoa na vitendo vyao kwa jumla.Inasikitisha kuwa badala ya kufahamu uzito wa kimaadili na kisiasa walio nao nchini, viongozi hao wawili wamerejelea mtindo wao wa kukashifiana hadharani, siku moja tu baada ya Kenya kumuaga Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Hata siku moja haikuisha! Kiafrika, huo ni mwiko! Ni sawa na watoto wa mzee aliyeaga kuanza kulumbana mara tu baada ya kumzika.

Mzee Kibaki alizikwa Jumamosi, huku wawili hao wakielekezeana lawama kwa matusi Jumapili.

Huu ni mfano mbaya ambao viongozi hao wanawawekea Wakenya na vizazi vinavyowatazama.

Ni sawa na kumkosea heshima Mzee Kibaki, ikizingatiwa kuwa katika safari yake ya kisiasa, alikuwa mtu aliyezingatia amani na utulivu mkubwa.

Hata ikiwa Rais Kenyatta na Dkt Ruto wana tofauti zao za kisiasa, wangengoja angaa familia ya Mzee Kibaki kumwomboleza mpendwa wao kwa siku kadhaa ndipo waanze tena mieleka yao ya kisiasa.

Kamwe, hili ni kosa lisilosameheka hata kidogo.