Connect with us

General News

Rivatex yataka wakuzaji waboreshe kilimo cha pamba – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Rivatex yataka wakuzaji waboreshe kilimo cha pamba – Taifa Leo

Rivatex yataka wakuzaji waboreshe kilimo cha pamba

NA BARNBAS BII

KIWANDA cha kutengeneza nguo cha Rivatex, mjini Eldoret, kimezindua mpango wa kuhakikisha kuwa wakulima wanakiwasilishia pamba bila changamoto zozote wakati huu ambapo kinalenga kuimarisha oparesheni zake ili zifikie viwango vya kimataifa.

Kupitia mpango huo, usimamizi wa Rivatex, umewafikia wakulima katika maeneo yanayokuza pamba ya Mashariki na Magharibi mwa Kenya ili kuwahimiza washiriki kilimo hicho kwenye ekari kadhaa za ardhi.

Rivatex inaona hatua hiyo kama mbinu ya kuongeza uzalishaji na kumaliza tatizo la kukosa pamba wakati wa oparesheni zake.

“Tunawapa wakulima mbegu za kisasa na pia soko la kuuza mazao yao kwa bei ya juu ndipo wafaidike. Hii pia ni mbinu ya kuwahimiza wakumbatie kilimo cha pamba kwa wingi,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa Rivatex Profesa Thomas Kurgat.

Hitaji la pamba linatarajiwa litaongezeka sana baada ya serikali kuwekeza Sh650 milioni kuimarisha miundombinu na utendakazi wa Rivatex ambacho ni kiwanda pekee kinachotengeneza nguo Bonde la Ufa.

Katika bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha Ukur Yattani kwenye bajeti ya 2022/23, kiwanda hicho kilitengewa Sh410.4 milioni na Sh212.1 milioni zikitengewa viwanda vingine vidogo vinavyotengeneza nguo nchini.

Vilevile, Bw Yattani alitenga Sh250.4 milioni kufufua sekta ya kilimo cha pamba kwenye bajeti hiyo iliyosomwa wiki jana.

Hapo awali, usimamizi wa Rivatex ulikuwa umelalamikia kuwa utendakazi wake haujakuwa ukiendelea vyema kutokana na ukosefu wa pamba. Kiwanda hicho kinahitaji robota 70,000 za pamba kila mwaka ilhali kimekuwa kikipata tu robota 40,000.

Hata hivyo, Rivatex inalenga kuongeza kiwango cha pamba kinachotumia kila siku kutoka robota 10,000 hadi robota 100,000. Hii inafasiriwa kuwa watakuwa wanatumia mita 40,000 kutengeneza nguo kutoka mita 5,000 kila siku.

Ili kutimiza malengo hayo, wakulima nao watahitajika wajizatiti kwa kuwa kilimo hicho kinafaa kuendelezwa katika ekari 50,000 za ardhi.

Eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa pekee lilitoa tani 852.60 za pamba kwenye ardhi ya ekari 794.5.

Prof Kipkurgat alisema kuwa kiwanda hicho kinashirikiana na kaunti za Mashariki na Magharibi kuongeza kiwango cha uzalishaji wa pamba. Kati ya kaunti zinazowasilisha pamba kwa wingi ni Kisumu, Homa Bay, Bungoma, Baringo na Tana River.

Kenya huzalisha tani 5,300 za pamba ilhali mahitaji ni tani 38,000 huku serikali ikitumia Sh17 bilioni katika kununua pamba kutoka mataifa jirani.

Kiwanda cha Rivatex kilipata mkopo wa Sh3 bilioni miaka mitatu iliyopita kutoka serikali ya India pamoja na Sh3 bilioni zilizopokezwa na Hazina Kuu ya Kifedha ili itengeneza mashine zake zilizoharibika.

Rivatex ilinunuliwa na Chuo Kikuu cha Moi kwa kima cha Sh205 bilioni baada ya kuwekwa chini ya mrasimu miaka 10 iliyopita kutokana na changamoto za kifedha zilizokuwa zikiikumba.