Rotich aonya wapinzani mita 800 akielekea Botswana kujinoa
Na AYUMBA AYODI
MSHINDI wa medali ya fedha ya Olimpiki mbio za mita 800 Ferguson Rotich atatumia shindano la Gaborone International Meet nchini Botswana hapo Aprili 30 kujiandaa shindano la Absa Kip Keino Classic litakalofanyika Mei 7 uwanjani Kasarani.
Rotich hakuhudhuria mashindano ya kitaifa ya Kenya yaliyofanyika Aprili 26-28 ugani Kasarani ili ajiandae vyema kwa shindano hilo la Gaborone ambalo ni la kiwango cha shaba kwenye mashindano ya Shirikisho la Riadha Duniani. Kip Keino Classic ni kiwango cha dhahabu.
“Ambia wapinzani wangu kuwa nitarejea kunyakua taji langu la Kip Keino Classic,” alionya Rotich, 32, anayepanga kusafiri Ijumaa.
Rotich, ambaye aliambulia nishani ya shaba kwenye Riadha za Dunia 2019 nchini Qatar, alitwaa taji la Kip Keino mnamo Oktoba 3, 202o, lakini akatupwa hadi nambari tano mnamo Septemba 18, 2021.
“Sikuwa nahisi vizuri mwaka jana, lakini nililazimika kukimbia tu kwa sababu ilikuwa nyumbani,” alifichua Rotich ambaye shindano la Gaborone ni lake la kwanza mwaka huu.
“Nimejiandaa vyema na bado napiga msasa kasi yangu ya kumalizia mbio na pia uvumilivu. Nataka kupima ni wapi naweza kushambulia vyema wakati wa mbio,” alieleza Rotich aliyeongeza kuwa anatumai kupata matokeo mazuri Gaborone na Kip Keino Classic, miongoni mwa mbio nyingine msimu huu.
Rotich atapimwa vilivyo na mwenyeji na bingwa wa michezo ya Jumuiya ya Madola mbio za mita 800 Amos Nijel, miongoni mwa wengine jijini Gaborone.
Rotich aliongeza kuwa anafurahia kuimarika kwake kutoka nishani ya shaba kwenye Riadha za Dunia 2019 hadi medali ya fedha kwenye Olimpiki 2020.
“Hiyo grafu imenifurahisha na ninatumai mambo yatakuwa mazuri zaidi mwaka huu,” alieleza Rotich anayetumai kushiriki duru za Riadha za Diamond League za Doha (Mei 13) na Birmingham (Mei 21).
Lengo lake kubwa 2022 ni kushiriki Riadha za Dunia nchini Amerika mnamo Julai 15-24 na Jumuiya ya Madola mnamo Julai 28 hadi Agosti 8.
TAFSIRI: GEOFFREY ANENE
Next article
Kikao cha Kibaki chageuzwa uwanja wa Azimio na Kenya Kwanza…