Connect with us

General News

Ruto acheza karata ya mwaniaji mwenza – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Ruto acheza karata ya mwaniaji mwenza – Taifa Leo

Ruto acheza karata ya mwaniaji mwenza

NA BENSON MATHEKA

UAMUZI wa Naibu Rais William Ruto wa kumteua Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua kuwa mwaniaji mwenza wake kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9 umetajwa kama karata ya pata potea.

Wachaganuzi wanasema uteuzi wa Bw Gachagua unaweza kubomoa umaarufu ambao Dkt Ruto amejijengea eneo la Mlima Kenya na maeneo mengine nchini hasa kwa kukosa kumteua Seneta wa Tharaka Nithi, Kithure Kindiki ambaye alikuwa kifua mbele kwenye kura za maoni.

Wadadisi hao wanasema Bw Gachagua hana sifa kitaifa na maadili yake yametiwa doa na kesi za ufisadi zinazoendelea kortini dhidi yake.

Katika shtaka moja amekanusha kwamba alijipatia Sh6 milioni kutoka serikali ya Kaunti ya Nyeri akidai angeiuzia mashine za kusafisha damu.

Kwenye shtaka lingine inadaiwa alihusika na ulanguzi wa jumla ya Sh112 milioni kutoka kaunti za Bungoma na Kwale zilizopatikana kwa njia ya uhalifu.

Vile vile anakabiliwa na shtaka la kupata Sh7.3 bilioni kwa njia ya ulaghai kupitia akaunti yake katika benki ya Rafiki Micro-Finance Bank kati ya 2013 na 2020.

Mchambuzi wa siasa, Simon Gichuki anasema kwa kumteua Bw Gachagua akifahamu ana kesi za ufisadi mahakamani, Dkt Ruto amewapatia wapinzani wake silaha ya kumshambulia nayo.

“Ruto amefungulia wapinzani wake milango ya kumshambulia. Kuanzia sasa, kampeni zitabadilika na kuathiri kwa kiwango kikubwa umaarufu wa Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya,” aeleza Bw Gichuki.

Mdadisi huyu anasema umaarufu wa Bw Gachagua hauwezi kulinganishwa na wa washirika wengine wa Dkt Ruto kutoka eneo la Mlima Kenya waliopigiwa upatu kuwa wagombea wenza wake.

“Nafikiri Ruto hakushauriwa ipasavyo kwa kumteua mtu ambaye hana sifa kitaifa, na kumuacha msomi kama Kindiki ambaye uadilifu wake haujatiliwa shaka,” aongeza.

Kura za maoni za wiki jana zilionyesha kuwa wafuasi wengi wa Dkt Ruto walimpenda Prof Kindiki, Musalia Mudavadi au Anne Waiguru kuwa mgombea mwenza wake.

Jina la Bw Gachagua halikuwa miongoni mwa waliopendelewa na wapigakura.

Duru zinasema pia kura za maoni za chama cha Dkt Ruto cha United Democratic Alliance (UDA) zilionyesha Bw Gachagua akiwa nyuma ya Profesa Kindiki, Waiguru na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi.

MANUNG’UNIKO

Dalili kwamba huenda uamuzi wa Dkt Ruto ukazua mgawanyiko miongoni mwa washirika wake mlimani zilionekana Jumapili Prof Kindiki aliposusia hafla ya kumtangaza Bw Gachagua.

Wachaganuzi wanasema pia kuna uwezekano mkubwa wa Dkt Ruto kupoteza kura eneo la Mlima Kenya Mashariki anakotoka Prof Kindiki kufuatia kutoteuliwa kwake licha ya kuonekana kama ‘aliyefaa zaidi’.

Bw Gichuki anasema huenda Dkt Ruto alitekwa na idadi ya kura za eneo la Mlima Kenya Magharibi anakotoka Bw Gachagua na kusahau kwamba anahitaji pia za eneo la Mlima Kenya Mashariki.

Mara baada ya Dkt Ruto kumtangaza Bw Gachagua, wakazi wa Mlima Kenya Mashariki walilalamika wakidai kusalitiwa.

Kwa upande mwingine, mchaganuzi wa siasa Abraham Kimani anasema tofauti na wengine waliomezea mate wadhifa huo, Bw Gachagua ana uwezo wa kufadhili kampeni za Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya.

UWEZO KIFEDHA

“Atasaidia Dkt Ruto ikizingatiwa ana uwezo wa kifedha wa kuendesha kampeni na ana ujasiri wa kukabili wapinzani. Pili, Dkt Ruto alitaka mtu anayeweza kuibua msisimko miongoni mwa wapigakura,” asema Bw Kimani.

Anasema tajiriba ya Bw Gachagua katika siasa, utumishi wa umma, biashara na utawala pia itamsaidia Dkt Ruto katika kuendesha serikali iwapo watashinda.

“Ninamjua Rigathi kama mwanasiasa mwenye msimamo mkali katika masuala ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na pia kiongozi mweledi katika kufanya maamuzi,” alisema Bw Kimani.

Mchanganuzi huyo anasema kwa kumchagua Bw Gachagua badala ya Profesa Kindiki, Dkt Ruto ‘alivuruga hesabu ya mpinzani wake mkuu Raila Odinga’ ambaye anatarajiwa kutaja mwaniaji wake leo Jumatatu.

Akimtangaza kuwa mwaniaji mwenza wake, Dkt Ruto alisema kwamba amekuwa na Bw Gachagua tangu alipoanza safari ya kampeni yake ya hasla miaka minne iliyopita na kumtaja kama mwanasiasa na mfanyabiashara aliyefaulu mno.

Ili kufurahisha wapigakura wa Mlima Kenya ambao wamelalamika kuwa mkataba wa Kenya Kwanza umewatenga, Dkt Ruto aliahidi kumtwika Bw Gachagua majukumu makubwa ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi ya serikali.

Wengine waliokuwa wakipigiwa upatu wa kuwa naibu wa Dkt Ruto ni Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na mwenzake wa Kandara Alice Wahome.

Dkt Ruto aliwasifu hao wote akisema wana uwezo wa kuimarika kisiasa na katika kutumikia taifa.