Ruto apaka Uhuru tope Amerika
NA LEONARD ONYANGO
NAIBU Rais William Ruto ametumia ziara yake Amerika kumshambulia vikali Rais Uhuru Kenyatta na kuyataka mataifa ya Magharibi kumsaidia kuchunga kura zake zisiibwe na serikali.
Akizungumza jana katika Chuo Kikuu cha Loyola, Maryland, Dkt Ruto alidai Rais Kenyatta amewatenga maskini katika uchumi na kunufaisha mabwanyenye.
“Hiyo ndiyo maana muungano wa Kenya Kwanza unalenga kuhakikisha uchumi wetu unaboresha maisha ya kila Mkenya na wala si mabwanyenye wachache,” akasema Dkt Ruto ambaye ameandamana na ujumbe wa watu 31, akiwemo mkewe Rachel na kinara wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi. Ziara hiyo ya siku 10 ughaibuni imegharimu Wakenya Sh107 milioni.
Naibu Rais alishutumu serikali ya Rais Kenyatta kwa kutumia ‘kifua na vitisho kujaribu kuingiza kinara wa ODM Raila Odinga mamlakani.
Alidai serikali inatumia taasisi mbalimbali kuhangaisha baadhi ya wanasiasa na kutishia raia ‘kupigia kura mtu fulani’.
“Kenya ni nchi yenye demokrasia. Lakini wasiwasi tulio nao ni kwamba, kuna baadhi ya watu watatumia kifua kujaribu kubadili uamuzi wa Wakenya kupitia wizi wa kura.
“Matumaini yangu ni kwamba, Wakenya hawatakubali kura kuibwa na watasimama imara. Hawatakubali kuchaguliwa viongozi. Mimi pia nitasimama imara kuhakikisha kura hazitaibiwa hata kama nitapoteza,” akasema Dkt Ruto.
Alidai Rais Kenyatta anafadhili vyama vidogo vya ‘kikabila’ kwa lengo la kugawanya nchi. “Nadhani hatua hiyo ya kufadhili vyama vidogo vya kikabila ni hatari kwa nchi. Athari za kuingiza ukabila kwenye siasa tunazijua vyema.
“Washindani wetu wamehisi kushindwa sasa na wamekumbatia vyama vya kisiasa vya kikabila lakini inaonekana Wakenya wamekataa,” akasema Naibu wa Rais.
Alisema Rais Kenyatta alikumbatia vyama vya kisiasa vya kikabila baada ya ‘kushindwa kusimamia vyema chama cha Jubilee kilicholenga kuunganisha Wakenya’.
“Usimamizi mbovu wa Jubilee ulitufanya kuhama na kuunda chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho kina sura ya kitaifa. Haitakuwa rahisi kwetu kufaulu lakini tutajitahidi kuhakikisha tunafikia malen – go yetu,” akasema Dkt Ruto.
Hata hivyo, Dkt Ruto alitumia miradi ambayo imetekelezwa na serikali ya Jubilee kujipigia debe.
“Tulikuwa na mpango mzuri kati ya 2013 na 2017. Tulitengeneza barabara za urefu wa kilomita 10,000. Tuliunganisha nyumba milioni 8.5 na umeme kutoka milioni 2.5. Tulitaka kufanya mengi kwa kuwezesha vijana kupata ujuzi na tulikuwa tumejenga vyuo vya ufundi 150,” akasema.
Kulingana na Dkt Ruto, hali ngumu ya uchumi imesababisha mamilioni ya vijana kushindwa kulipa mikopo wanayochukua kupitia simu au benki.
“Nchini Kenya, vijana wananyonywa kwa kutozwa riba ya juu na inasikitisha kwamba, kufikia sasa kuna zaidi ya Wakenya milioni 14 wamezuiliwa kuchukua mikopo kwa kushindwa kulipa ya awali,” akadai Naibu Rais.
Alikosoa mpango wa huduma nafuu za matibabu kwa wote (UHC) huku akisema unabagua baadhi ya Wakenya.
“Kwa sasa serikali inalipia bima ya afya (NHIF) Wakenya milioni 1.5. Lakini mimi nikiingia mamlakani nitahakikisha kuwa Wakenya milioni 5 wananufaika na mpango huo,” akadai.
Dkt Ruto, hata hivyo, alikuwa na kibarua kigumu kujibu swali kuhusiana na madai ya kuhonga mashahidi wa kesi dhidi yake katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC).
“Shutuma za kuhonga mashahidi katika ICC zilikumba pande zote; upande wa mashtaka na upande wa utetezi hivyo sifai kulaumiwa. Lakini jambo la muhimu ni kwamba, mimi na Rais Kenyatta ambao tulishtakiwa tuliachiliwa huru na tukaongoza juhudi za kuunganisha Wakenya kwa kuunda serikali 2013,” akasema.
Naibu wa Rais anataelekea Uingereza Machi 5 ambapo atatoa hotuba katika taasisi ya Chatham House. Machi 8, Dkt Ruto ataelekea Qatar na kisha kurejea nchini Machi 11.