MABAHARIA saba kutoka Tanzania waliponea chupuchupu boti yao iliposombwa na mawimbi makali na kuzama kwenye Bahari Hindi eneo la Shanga, Kaunti ya Lamu.
Ilibainika kuwa saba hao walikuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam, Tanzania kuelekea Kismayu, Somalia kuchukua mzigo wa vyuma vikuukuu ajali hiyo ilipotokea.
Walitambuliwa kama Swaleh Ramadhani Katambo, Mganga Mgoya, Abas Muharami, Msafiri Abdallah, Omari Jalala, Ibrahim Matoye Tumaini na Mohamed Salim.
Akithibitisha ajali hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ulinzi wa Fuo za Bahari (KCGS), Bw Loonena Naisho alisema maafisa wake kwa ushirikiano na wanajeshi wa majini walifaulu kuwaokoa mabaharia hao saba wote wakiwa hai pamoja na mizigo yao.
Afisa Mkuu wa Kenya Coast Guard Service (KCGS), Loonena Naisho akihutubu. Amethibitisha kuokolewa kwa saba hao kwenye Bahari Hindi eneo la Lamu. Picha/ Kalume Kazungu
Boti yao kwa jina MV Al Feroz ilizama baharini na hadi kufikia wakati wetu kwenda mtamboni ilikuwa bado haijapatikana.
Bw Naisho aliwashauri watumiaji wa bahari kuwa waangalifu na kuepuka sehemu za bahari ambazo zinatambulika kwa kina kirefu hasa msimu huu ambapo bahari inashuhudia upepo na mawimbi makali.
“Tukitii hayo maelekezo tutaepuka hizo ajali, maafa na mali kuharibikia baharini,” akasema Bw Naisho.
Msemaji wa mabaharia hao, Bw Swaleh Ramadhani Katambo alishukuru vyombo vyote vya usalama vya Kenya vilivyohusika kuwaokoa wakati ajali ilipotokea.
“Tuliwapigia simu na baada ya muda mfupi wakafika kutuokoa. Japo boti yetu ilizama lakini twafurahia kwamba tuko hai,” akasema Bw Katambo.
Bw Mganga Mgoya alishukuru uhusiano uliopo kati ya Kenya na Tanzania, akiutaja kuwa kigezo mojawapo kilichosukuma wao kupata usaidizi wa haraka walipokumbwa na tatizo baharini.
Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia pia aliahidi kwamba raia wa Tanzania waliookolewa watasaidiwa kurudi nchini kwao.
Bw Macharia aidha aliwashauri mabaharia kuzingatia maonyo yanayotolewa kuhusiana na hali ya hewa na bahari ili kuepuka kuendeleza safari baharini nyakati mbaya.