Sekta ya kibinafsi kusaidia kuzima vikwazo katika biashara
NA KENYA NEWS AGENCY
SEKTA ya kibinafsi katika mataifa ya Kenya na Uganda itachangia nafasi muhimu kusaidia nchi hizo mbili kukomesha Vikwazo vya Kodi (NTBs) vinavyoathiri biashara kati ya mataifa hayo.
Chama cha Kitaifa kuhusu Wafanyabiashara na Viwanda Nchini (KNCCI), tawi la Mombasa, mnamo Jumatano, kilitia saini mkataba na Uganda unaodhamiriwa kuondoa vizingiti vinavyolemaza ukuaji wa biashara na uwekezeji.
Mkataba huo uliowekwa saini na Mwenyekiti wa KNCCI tawi la Mombasa, Bw Mustafa Ramadhan na Balozi wa Uganda mwenye makao yake Mombasa, Jenerali Paul Mukumbya, unapatia kipaumbele ushirikiano kuhusu kilimo na bidhaa za kilimo kwa minajili ya ukuaji na manufaa kwa nchi hizo mbili.
“Mkataba wa ushirikiano uliowekwa saini hii leo ni ishara ya ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili kwa ukuaji na manufaa kwa mifumo ya uchumi nchini Kenya na Uganda hasa kupitia sekta ya kilimo na kilimobiashara ambazo kando na kutumika kama vichocheo vya kuendeleza mahusiano kati ya Kenya na Uganda, vilevile ni nyenzo za kuwezesha ustawi kwa mataifa haya mawili,” ilisema taarifa ya pamoja.
Balozi Mukumbya alisema ushirikiano huo ni sehemu ya hatua za ufuatilizi zilizoafikiwa kuchukuliwa baada ya kongamano kuhusu kilimo biashara lililofanyika mwaka jana, Mombasa, ambapo mbinu za kusuluhisha NBTS zinazoathiri mtiririko wa biashara kati ya nchi hizi mbili zilijadiliwa.
Kongamano hilo lililokuwa na kaulimbiu -”Kufungua uwezo wa kilimobiashara ili kupiga jeki uuzaji kwa mataifa ya kigeni”, lilihudhuriwa na wadau zaidi ya 500 wa sekta za kibinafsi na za umma.
Waziri wa Viwanda, Bi Betty Maina na mwenzake wa Uganda Francis Mwembesa, walihudhuria hafla hiyo iliyowaleta pamoja wadau wa kilimo na kilimo biashara, ikiwemo miungano na vyama vya mashirika ya wakulima na watowaji huduma za kifedha.
Balozi wa Uganda aliashiria kuwa serikali za nchi hizo mbili zimekubaliana kushirikiana na wadau wa sekta za kibinafsi, kusaidia kukomesha vizingiti vya kodi kwenye mpaka kati ya Kenya-Uganda ili kurahisisha biashara kati ya mataifa hayo mawili.
“Hapo awali, tulikuwa tunaketi kama serikali na kukabiliana na masuala yanayoathiri biashara katika sekta ya kibinafsi. Hivyo basi, tumeona haja ya kujumuisha wadau wa sekta ya kibinafsi kusaidia kusuluhisha matatizo hayo,” alisema.
Next article
Mchujo: Joho akosoa msimamo wa Shahbal