Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja amejiuzulu kama mwenyekiti wa kamati ya pamoja inayoshughulikia janga la ugonjwa wa corona
Haya yanajiri saa chache tu baada ya seneta huyo kuandikisha taarifa katika kituo cha polisi cha Kilimani kufuatia ukiukaji wa sheria ziliowekwa na serikali za kutotoka nje baada ya saa tatu usiku.
Sakaja pamoja na wenzake watatu walikamatwa Jumamosi, Julai 18 mwendo wa saa nane usiku wakiburudika kwa vileo saa za kafya.
Seneta huyo ameomba msamaha kwa kukaidi amri ya kafyu huku akihoji kuwa kila binadamu kufanya makosa kwa njia moja au nyingine.
” Nakubali kuvunja sheria ya kutotoka nje iliyowekwa kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya COVID-19, nilikuwa nje ya nyumba yangu siku ya Ijuma kinyume na sheria, najutia ila yameshatendeka, hata hivyo, kila binadamu hufanya makosa,” Alisema Sakaja.
” Ningependa kuwaomba Wakenya msamaha, nakubali kukabiliwa kisheria, ningependa pia kujiuzulu kama mwenyekiti wa kamati ya seneti inayoshughulikia janga la corona, tayari tumefanya kazi nzuri kufikia sasa na ninaunga mkono juhudi za serikali katika kupigana vita dhidi ya janga hili,” Aliongezea Sakaja.
Sakaja aliachiliwa kwa dhamana ya KSh 10,000 na atafikishwa katika mahakama ya wazi ya Kasarani Jumanne, Julai 21.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsaApp: 0732482690.