TAHARIRI: KCPE: Serikali ihakikishe kila mtoto anafanya mtihani wake
NA MHARIRI
KWA siku tatu zijazo, wanafunzi milioni moja na laki mbili watafanya mtihani wa kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) katika vituo 28, 316.
Mtihani huo utakuwa ni kilele cha juhudi zao za miaka zaidi ya minane katika shule ya msingi. Mbali na miaka mitatu ya chekechea, watahiniwa hao pia walipoteza mwaka mzima wakiwa nyumbani kutokana na janga la Covid-19.
Kwa sababu ya changamoto hizo, Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha aliahidi kuwa mtihani huu unaoanza leo Jumatatu, ulitungwa kwa kuzingatia hali ambayo wanafunzi hao wamepitia. Haitarajiwi kuwa utakuwa mgumu sana, kwa kuwa hatimaye serikali inatarajia watahiniwa wote wajiunge na shuleza upili.
Mtihani unafanywa wakati ambapo kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Agosti zinaendelea.
Huu ni wakati ambapo wanasiasa wanapaswa kuelewa umuhimu wa siku hizi tatu kwa watoto wetu. Ikiwezekana, wanapaswa kuahirisha kampeni zao hadi Alhamisi. Wanasiasa wengi hutumia vituo vya biashara na viwanja ambavyo katika maeneo mengi ya nchi, huwa karibu na shule za msingi.
Kwa kukatiza kampeni kwa siku hizo tatu, viongozi hao watadhihirishia kwamba kweli wanapenda maendeleo ya watoto. Bila hivyo, ahadi zao za kuboresha elimu kwa kujenga madarasa na kadhalika hazitakuwa na maana.
Lakini mtihani huu pia unafanywa huku baadhi ya maeneo Rift valley, Mashariki na Maskazini Mashariki yakikumbwa na utovu wa usalama. Baadhi ya maeneo hayo ni Kaunti ya Baringo, ambako watu saba waliuawa Jumamosi usiku. Isiolo, watu 11 wameuawa kwa muda wa siku mbili. Kuna mashambulizi ya kila mara katika Bonde la Kerio kati ya maeneo mengine.
Prof Magoha amehakikishia nchi kwamba kutakuwa na helikopta za kutosha kupeleka mitihani katika maeneo yanayokumbwa na changamoto za kiusalama.
Tangazo hili linaweza kuchukuliwa kuwa serikali haijali maisha ya wanafunzi na walimu katika maeneo hayo.
Kusema kwamba heliopta zitapeleka mitihani, ni sawa na kusema kwamba kilicho muhimu kwa serikali ni mtihani ufanywe, bila kujali kama wanafunzi na walimu wao watavamiwa na majangili au la.
Ni kweli kwamba mtihani ni muhimu na lazima kila mtahiniwa aliyesajiliwa, aufanywe. Lakini serikali kwanza ihakikishe kila mtoto na msimamizi wa KCPE yuko salama.
Itakuwa makosa kwa watoto katika maeneo yasiyo na usalama wa kutosha kukosa kuufanya mtihani, eti kwa sababu serikali haikujipanga mapema kuweka mazingira salama.