[ad_1]
WANTO WARUI: Serikali itafute chanzo cha matokeo duni katika baadhi ya shule nchini
NA WANTO WARUI
MATOKEO ya mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) yaliyotangazwa juma lililopita na Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha yalipokelewa kwa shangwe na idadi ndogo tu ya wanafunzi waliopata alama za kuridhisha.
Wanafunzi wengi sana walisononeka kutokana na kile walichokiita kutoridhika na matokeo yao. Wengi wao ni wale waliopata alama kati ya 380 – 399 kwani walitarajia kuwa wangeweza kupata alama mia nne.
Kuna shule zilizotokea barabarani kwa ving’ora hasa katika miji mikuu zikijitanua kifua kwa matokeo bora. Nyingi za shule hizi ni zile za kibinafsi.
Ni kweli kuwa, watu wengi huamini shule za kibinafsi hufanya vizuri kutokana na sababu kuwa zina vifaa bora ikilinganishwa na zile za umma. Lakini matokeo bora hayategemei vifaa zaidi kuliko utendakazi.
Sababu kuu ya shule za kibinafsi kujizolea alama nzuri ni usimamizi bora, maandalizi ya kina, utendakazi mzuri , ushirikiano wa wazazi na walimu na nidhamu.
Katika shule nyingi za umma, mambo haya hukosa. Ukitembea katika baadhi ya shule za umma ambazo huzoa alama nzuri, kwa mfano shule ya msingi ya D.E. B Karatina au Kathigiriri B, utakuta shughuli za masomo katika shule hizo ni tofauti kabisa na za shule nyingine.
Walimu hujitolea katika utendakazi wao, wazazi hujitolea katika kuwajibikia masomo ya watoto wao na wanafunzi huzingatia nidhamu kikamilifu. Hii ndiyo sababu ambayo hufanya shule hizo zifanye vizuri ikilinganishwa na nyingine za umma.
Kulingana na Waziri wa Elimu, George Magoha, asilimia 47 ya wanafunzi walipata kati ya alama 200 – 299.
Ni vyema serikali ichunguze kiini cha matokeo duni!
[ad_2]
Source link