Serikali yataja mkakati wake kuwasaidia waathiriwa wa baa la njaa
Na LAWRENCE ONGARO
SERIKALI imetangaza itaendelea kuwafaa watu walioathiriwa na baa la njaa katika kaunti tofauti nchini.
Waziri wa Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Profesa Margaret Kobia, alisema serikali tayari imepeleka tani 40 za chakula kwa familia 6,500 zilizoko eneo la Kaskazini Mashariki.
Alisema serikali ya Kuwait nayo imejitolea kuisaidia Kenya na kuipa chakula hicho ili kuwafikia walioathirika.
Prof Kobia alieleza kuwa tayari watu wapatao 2.5 milioni wameathirika na janga hilo la njaa.
“Serikali itatuma maafisa wake mashinani kuhakikisha kuwa chakula hicho kinanufaisha kila mmoja aliyeathirika. Machifu na maafisa wa serikali watakuwa mstari wa mbele kusimamia shughuli hiyo,” alisema Prof Kobia.
Alisema serikali itahakikisha inawahamasisha wakazi wa maeneo yaliyoathirika ili waweze kujisimamia wenyewe.
Lori la chakula cha msaada. PICHA | LAWRENCE ONGARO
Pia serikali itachimba visima vya maji ili kuhakikisha wakazi wa maeneo hayo hawakosi maji wakati wa kiangazi.
Wakazi hao pia watahamasishwa kuhusu unyunyuziaji wa maji kwenye mashamba yao.
Alieleza baadhi ya maeneo yatakayonufaika na chakula hicho cha msaada ni Marsabit, Turkana, Wajir, Garissa na Samburu.
Waziri huyo alisema serikali imetenga takribani Sh8.5 bilioni za kuzinufaisha familia zilizoathirika katika kaunti 13 kote nchini.
Alieleza kuwa serikali ina mipango ya kunufaisha wazee kupitia kwa fedha za Inua Jamii.
Wakati huo huo pia serikali imetenga Sh400 milioni za biashara ili kuwanufaisha wanafunzi ambao hawana uwezo wa kulipa karo.
Balozi wa Kuwait aliye hapa nchini Bw Qusia Al-Farham, alisema nchi yake itaendelea kuisaidia Kenya kwa hali na mali.
Kuwait imetoa mchango wa chakula kama mchele, mahindi, sukari na hata mafuta ya kupikia.
Alieleza kuwa chakula hicho kitatosheleza waathiriwa kwa zaidi ya miezi miwili.
Balozi huyo alisema ushirikiano wa Kuwait na Kenya ni wa muda mrefu na kwa hivyo watazidi kuisaidia kwa vyovyote vile.