Connect with us

General News

Serikali yaweka kafyu ya siku 30 kukabili uvamizi Lamu – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Serikali yaweka kafyu ya siku 30 kukabili uvamizi Lamu – Taifa Leo

Serikali yaweka kafyu ya siku 30 kukabili uvamizi Lamu

Na MARY WAMBUI

SERIKALI imetangaza kafyu ya siku 30 katika kaunti za Lamu Magharibi na Kati kuhusiana na kudorora kwa usalama ambapo watu saba wameuawa na wanamgambo wa Al-Shabaab tangu Jumapili.

Kafyu hiyo itakayoanza leo itaathiri maeneo ya Majembeni, Ndamwe na Mkunumbi katika Kata ya Mkunumbi, Pandanguo, Binde Warinde, Witu na Kata ya Hamasi eneo la Witu.

Maeneo mengine ni pamoja na Bomani, Pongwe, Mpeketoni, Bahari na Mapenya katika Kata ya Mpeketoni na eneo la Hindi, Lamu ya Kati.

“Kulingana na Kifungu 106 (1) cha Sheria kuhusu Huduma ya Polisi 2011, Baraza la Kitaifa kuhusu Usalama limetangaza maeneo yafuatayo kama yenye utata na kuamrisha kafyu ya kuanzia jioni hadi alfajiri kwa muda wa siku 30 kuanzia Januari 5, 2022,” ilisema taarifa kutoka kwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i.

Waziri Matiang’i alisema kuwa Baraza la Kitaifa kuhusu Usalama vilevile limeagiza kutumwa mara moja kwa timu ya vikosi mbalimbali vya walinda usalama kukusanya silaha na kukomesha shughuli haramu katika maeneo yaliyoathirika.

Wakazi wanaoishi katika maeneo yaliyotangazwa hivyo basi wanahitajika kushirikiana na vikosi vya usalama na kusambaza habari kuhusu watu na shughuli za kutiliwa shaka.

Taharuki imetanda katika kaunti hiyo tangu Jumapili usiku wakati wanamgambo wa Al-Shabaab walipowaua watu sita katika kijiji cha Witho na nyumba kadhaa kuteketezwa kwenye shambulizi hilo.

Miongoni mwa wahasiriwa ni mmiliki wa kituo cha kuuzia pombe pamoja na wasaidizi wake waliofungwa mikono kabla ya kuteketezwa.

Wengine wawili ni pamoja na mzee wa kijiji na mkazi mmoja waliokatwa kichwa na kupigwa risasi mtawalia.Watu wengine wawili hawajulikani walipo baada ya kudaiwa kutekwa nyara na wanamgambo hao.

Kamanda wa Polisi, Kaunti ya Lamu, Moses Muriithi alithibitisha kuwa wawili hao walitekwa nyara katika eneo la Kibokoni, LamuMagharibi mwendo wa saa kumi na moja jioni, mnamo Jumanne.

‘Tulipokea ripoti kutoka kwa mgemaji divai kwamba walikuwa wamekwenda kugema mkoma walipotekwa nyara na watu wasiojulikana. Mmoja wao alitoweka na anatusaidia kuwasaka wawili waliosalia ambao bado hawajulikani walipo. Msako unaendelea,” alisema Bw Muriithi.

Matukio hayo yamewaacha wakazi wakihofia mashambulizi na kutekwa nyara huku wito ukitolewa wa kuimarisha usalama eneo hilo.