Mchujo: Shahbal, Nassir walumbania tiketi ODM
NA WAANDISHI WETU
MZOZO umeibuka kati ya mfanyabiashara, Bw Suleiman Shahbal, na Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, kuhusu tikiti ya Chama cha ODM ya kuwania ugavana Mombasa.
Hii ni baada ya kubainika kuwa, kura ya maoni iliyodhaminiwa na ODM ilionyesha Bw Nassir ana umaarufu kumliko Bw Shahbal katika uwaniaji ugavana.
ODM inategemea kura za maoni kama mojawapo ya mbinu za kuamua anayestahili kupeperusha bendera ya chama katika uchaguzi wa nyadhifa mbalimbali kote nchini.
Wiki iliyopita, chama hicho kiliahirisha kura ya mchujo iliyopangiwa kufanyika Mombasa na Kilifi ili kutoa muda zaidi wa mashauriano kuhusu wagombeaji ambao wanaweza kuelewana kuachia wenzao nafasi.
Bw Shahbal jana alipinga utumizi wa kura za maoni akisisitiza kuwa mbinu hiyo haina uaminifu.
Akizungumza alipokutana na wanachama wengine Mombasa wanaopinga kura za maoni, alisema kura ya mchujo pekee ndiyo inawapa wananchi nafasi ya kujiamulia viongozi wanaowataka kwa njia ya haki.
Alimtaka kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, atimize ahadi yake kwa wanachama kuwa kutakuwa na uteuzi wa haki.
“Bw Odinga alitushika mkono na Bw Nassir katika uwanja wa Tononoka na kuahidi uteuzi huru na wa haki, hilo ndilo tunaloomba. Tuko tayari kwa uteuzi. Kama unajiamini na kura za maoni, unaogopa nini? Tukutane kwenye debe ili tujue mbivu na mbichi,” akasema.
Bw Shahbal ameonya kuwa ODM inaweza kupoteza viti katika ngome zake iwapo itashindwa kushughulikia suala la uteuzi kwa umakini.
“Tutasimama na Bw Odinga na kuhakikisha anashinda urais lakini hapa Mombasa mtu yeyote asijaribu kufanya maamuzi kwa niaba yetu. Haitatokea. Tumekataa kura za maoni ambazo zimefanywa hivi,” akasema.
Imebainika kura za maoni i zilifanywa katika wiki za kwanza za Februari na Machi.
Katika kinyang’anyiro cha ugavana, ilisemekana Bw Nassir alikuwa akiongoza kwa asilimia 36 huku Bw Shahbal akiwa na asilimia 27.
Bw Nassir alisema yuko tayari kukumbatia mbinu yoyote ya mchujo ambayo ODM itaamua kutumia, akisema anaamini atashinda kwa njia yoyote ile.
“Tunashukuru ODM kwa kuahirisha kura ya mchujo ili kutoa nafasi ya maelewano. Kwa wapinzani wangu, sisi sote ni wanaume tushindane lakini mjue hamtaweza kunishinda. Chama kiliwasikiliza na kuandaa kura ya pili ya maoni kwa sababu yao lakini wakasisitiza wanataka kujua kampuni gani iliyofanya utafiti. Huo ni mzaha, chama kina maarifa,” akasema.
Katika Kaunti ya Kilifi, Mwenyekiti wa ODM eneo hilo alibainisha kuwa tayari kuna maelewano baina ya waliotaka tikiti ya kuwania ugavana.
Tikiti hiyo ilikuwa ikiwaniwa na aliyekuwa waziri msaidizi wa ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, Naibu Gavana Gideon Saburi, aliyekuwa balozi wa Kenya nchini Tanzania Dan Kazungu, Spika wa Bunge la Kaunti Jimmy Kahindi, na waziri msaidizi wa zamani Francis Baya.
Katika Kaunti ya Taita Taveta, Mwanachama wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi katika ODM, Bw Richard Tairo, alithibitisha kuwa kura ya mchujo itaandaliwa katika Wadi za Mwatate na Mbololo pekee kwani wagombeaji walikubaliana kwenye nyadhifa nyinginezo.
Ripoti za Brian Ocharo, Winnie Atieno, Maureen Ongala na Lucy Mkanyika