Connect with us

General News

Shahidi adai msaidizi wa Jumwa alifyatua risasi 3 – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Shahidi adai msaidizi wa Jumwa alifyatua risasi 3 – Taifa Leo

Shahidi adai msaidizi wa Jumwa alifyatua risasi 3

NA BRIAN OCHARO

SHAHIDI wa pili katika kesi ya mauaji dhidi ya Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, jana Jumanne alieleza Mahakama Kuu ya Mombasa kwamba alishuhudia msaidizi wa mbunge huyo akifyatua risasi mara tatu wakati wa kisa hicho kilichotokea 2019.

Bi Jumwa na msaidizi wake, Bw Geoffey Otieno Okuto, walikuwa wamekanusha madai ya kuhusika kwa mauaji ya Jola Ngumbau katika boma la Bw Reuben Katana.

Marehemu alikuwa mjomba wa Bw Katana, ambaye alishinda uchaguzi mdogo wa Wadi ya Ganda kupitia kwa ODM.

Shahidi Joseph Kabwere alidai kuwa, alimuona Bw Okuto akichomoa bunduki na kufyatua risasi wakati mbunge huyo na wafuasi wake walipovamia boma la Bw Katana.

“Bw Okuto alipiga risasi kiholela, huenda risasi moja ndio ilimpata mwendazake. Alikuwa anafyatua risasi kuelekea mahali tulikuwa tukifanyia mkutano,” akasema shahidi huyo.

Shahidi wa tatu, konstebo wa polisi Sikuku Mayumbe, alisitishwa kuendelea kutoa ushahidi wake baada ya mawakili wa Bi Jumwa kulalamika hawakukabidhiwa stakabadhi alizotaka kueleza kuzihusu.

Afisa huyo wa polisi anatarajiwa kufafanua ripoti ya maelezo kuhusu jinsi eneo la mkasa lilivyokuwa.

Mawakili wa Bi Jumwa wakiongozwa na Bw Jared Magolo na Bw Danstan Omari, walidai kuwa uwasilishaji wa ushahidi ambao haujakabidhiwa kwao ni ishara kuwa upande wa mashtaka una nia mbaya katika kesi hiyo.

Wakili wa upande wa mashtaka, Bi Vivian Kambaga, alisisitiza ripoti hiyo iliwasilishwa kwa mawakili wa mlalamishi, lakini akakubali shahidi asiendelee kwa sasa kwani hakuna ushahidi wa kuthibitisha walipeana ripoti hiyo kwa upande wa Bi Jumwa.

Bw Kabwere alikuwa ni mmoja wa maajenti wa ODM waliokuwa katika boma la Bw Katana kupanga mikakati ya kulinda kura wakati wa uchaguzi huo mdogo.

Mahakama ilianza kupokea ushahidi wa upande wa mashtaka Jumatatu ambapo shahidi wa kwanza alithibitisha kuwa, mbunge huyo alikuwepo katika eneo la mkasa.

Bw Alfred Kahindi, ambaye pia wakati huo alikuwa ajenti wa ODM, alidai kushuhudia jinsi mbunge huyo, walinzi wake wawili na wafuasi wake walivyovamia boma la Bw Katana na kusababisha vurugu.

Kulingana naye, ilikuwa mwendo wa saa kumi jioni wakati yeye pamoja na maafisa wengine wa ODM walipokuwa kwenye mkutano wa kupanga mikakati ya uchaguzi mdogo wa wadi ya Ganda.

“Gari la polisi lilikaribia boma, maafisa wa chama waliondoka kwenye mkutano na kuzungumza kwa muda mfupi na maafisa hao kabla ya wao kuondoka,” akasema mbele ya Jaji Anne Ong’injo.

Alisema baada ya takriban dakika 20, gari lingine la polisi aina ya land cruiser lilirudi kwenye boma na baada ya muda mfupi prado mbili nyeupe zikafuata.

Kulingana na shahidi huyo, Bi Jumwa na walinzi wawili walishuka kutoka kwa magari hayo mawili.

“Nilimsikia Bi Jumwa akiwakashifu polisi kwa kukosa kufanya kazi ambayo alikuwa amewatuma kufanya, kisha akaapa kuifanya mwenyewe,” shahidi huyo alisema.

Alidai kuwa, hapo ndipo wafuasi wa Bi Jumwa walianza kurusha mawe akazidi kudai mbunge huyo aliamuru wafuasi wake kuchoma nyumba za Bw Katana.

Mahakama ilisikia kwamba waliokuwa katika boma la Bw Katana walianza kupambana na wafuasi wa Bi Jumwa.

Vurugu ziliendelea licha ya polisi kuingilia kati.Kulingana naye, polisi walifyatua risasi hewani na vitoa machozi kutawanya umati lakini hawakufaulu.

Shahidi huyo ambaye alikuwa akiongozwa katika ushahidi wake na Bi Kambaga, alisema aligundua Jola Ngumbao alipigwa risasi baada ya polisi kuwatawanya umati.

Alipohojiwa na upande wa mshtakiwa, Bw Kahindi alithibitisha kwamba ni Jumwa na msaidizi wake Bw Geoffrey Otieno Okuto waliovamia boma hilo.

Kulingana na upande wa mashtaka, kisa hicho cha mauaji kilitokea Oktoba 15, 2019.

Kesi hiyo ilikuwa imeahirishwa mara nyingi kutokana na sababu mbalimbali zilizoibuka kutoka kwa mawakili wa Bi Jumwa.