DOUGLAS MUTUA: Siasa kando, ya Ruto ni matusi ya kweli au utani kwa raia wa Congo?
NA DOUGLAS MUTUA
WAFUGAJI wa kisasa wana mzaha sana! Narejelea watu wanaofuga ng’ombe wa maziwa kwa ajili ya biashara.
Yaani wafugaji wanaouza maziwa yao viwandani, si wale wanaoyapikia chai, kuyalia ugali wala kuyagandisha mtindi.
Nimesema wafugaji hao wana mzaha kwa kuwa wanasema watu wanaofuga wale wenye nundu, ambao hurandaranda huku na kule wakitafuta malisho, hawana ng’ombe! Ni mtazamo kama huo ambao ulisababisha Naibu Rais, Dkt William Ruto, atanie kwamba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) haina ng’ombe hata mmoja.
Nia ya wanaofuga ng’ombe wa nundu si biashara bali tu fahari ya kuwa nao na kupata mbolea kwa ajili ya kilimo kidogo-kidogo.
Ipo ile desturi ya kuwa na ng’ombe mmoja au wawili usije ukaitwa maskini wa mwisho. Kwa maoni ya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa, hao si ng’ombe.
Labda ni punda. Wanakutambua ukifuga ng’ombe maridadi wa gredi, uwafungie zizini na kuwapelekea maji na malisho humo. Daktari wa minyoo, kupe na maradhi pia aje hapo kuwaona wagonjwa wake hao.
Hakika, utani ambao nimesikia tangu utotoni kutoka kwa wafugaji wa kisasa ni kuwa hao wenye nundu tunaoita ng’ombe ni wadogo sana hivi kwamba ukitaka kuwakama inabidi uwawekelee juu ya meza! Hebu msikilize mfugaji mkuu wa Uganda, Rais Yoweri Kaguta Museveni, akieleza sababu zake za kutokula kuku na samaki.
Anashikilia kuwa kuku ni mchafu kwani kawaida yake hula chochote anachookota hata kwenye jalala la takataka, naye samaki ni jamii ya nyoka!
Mzee wa watu anafunga kazi kwa kuuliza: “Nilijua halal zamani kuliko hao wanaosisitiza kula chakula halal. Nitakula ndege mchafu na nyoka kwa kukosa nini ilhali ng’ombe ninao?” Huo ni mtazamo ambao pia unashikiliwa na baadhi ya jamii za wafugaji nchini Kenya.
Nilicheka Wakongomani walipomjiia juu Dkt Ruto kwa kutania eti hawana ng’ombe. Nilijiuliza iwapo wako tayari kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo watalazimika kuvumilia utani na maudhi ya Wakenya.
Nilijiuliza iwapo walipitwa na mzaha wetu mtandaoni wakati wa michuano ya kabumbu ya African Cup of Nations (AFCON) mnamo 2019 pale Tanzania na DRC zilipoondolewa tukatania: Wanamuziki wamerejeshwa nyumbani.
Na je, hawajui ulimwengu wa Kiswahili hucheka nusura uteguke mbavu kila lahaja ya Kingwana – Kiswahili kinachozungumzwa DRC – inapohanikiza hewani? Naomba Afrika Mashariki tukomae, tuwe wakakamavu kikweli, tutaniane na kupendana kwa dhati ya nyoyo zetu.
[email protected]