Connect with us

General News

Siri za ukora ndani ya mtaa wa Makutano ulioko kaunti ndogo ya Mbeere Kusini – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Siri za ukora ndani ya mtaa wa Makutano ulioko kaunti ndogo ya Mbeere Kusini – Taifa Leo

Siri za ukora ndani ya mtaa wa Makutano ulioko kaunti ndogo ya Mbeere Kusini

NA MWANGI MUIRURI

KATIKA mtaa wa Makutano kuna mzunguko wa barabara za kuelekea miji ya Nyeri, Embu na Meru.

Hapo katika mtawanyiko wa barabara hizo, kuna siri kali za biashara haramu za ukahaba, wizi wa mafuta ya magari, usambazaji bangi, uchezaji kamari na upakiaji wa pombe haramu.

Kwa muda mrefu raia wamekuwa wakitoa malalamishi yao lakini ni kama vile serikali haijatilia maanani kero hiyo.

Ni mji mdogo uliojaa vumbi, takataka katika barabara za vichochoroni na maji taka ambayo hutoka katika vioo vya nyumba za makazi na kutapakaa barabarani huku biashara katika baa zikifanyika bila masharti yoyote ya kisheria.

Ni hivi karibuni ambapo kulizuka kilio cha wenyeji ambao waliteta kuwa kuna jumba moja la biashara ya ngono ambapo watoto wa shule walikuwa wakionekana wakiingia, hali ambayo polisi licha ya kujitokeza na kuahidi kuwa wangefuatilia kisa hicho, hakuna hatua ambayo imechukuliwa wiki moja baadaye.

“Huu ni mtaa wa karaha na hata mimi hufikiria kwamba tunaishi mfano wa watu wa Sodoma. Baadhi ya wenyeji ni wakora, baadhi ya maafisa wa polisi wetu ni wakora na serikali haijafanya jambo la kutosha kulainisha eneo hili,” anasema Bw Stephen Kaloki ambaye ameishi katika mtaa huo kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Anasema kwamba biashara ambazo huzolea wamiliki wazo faida katika mji huo ni zile za pombe na mihadarati, ukodishaji wa nyumba za malazi ikiwemo gesti, chakula na bidhaa za urembo.

Tony*, 25, ni mwanataaluma ambaye hajapata kazi katika kipindi cha miaka miwili sasa anasema aliingia katika mji huo na akazindua biashara ya kuuza madawa ya kuongeza nguvu za kiume “na kwa siku, kukiwa kumekauka kabisa, ni lazima niunde faida isiyopungua Sh1,000 kiasi kwamba hata sitafuti kazi ya taaluma yangu.”

Ni mji ambao baadhi ya makahaba wake wamejipanga vyema kwa kuwa 90 kati ya wote 302, huwa kila asubuhi wanachanga Sh200 kila mmoja na kumkabidhi mmoja wao akajiendeleze katika kile kinachofahamika vyema kama “merry-go-round”.

“Hiyo ina maana kuwa mmoja kati yetu kila asubuhi hukabidhiwa Sh18,000 ili akashughulikie mahitaji yake ya dharura na hata harakati za kujiendeleza. Hii ni baada ya kugundua kwamba shida kubwa ya wengi wetu ni kuwa na watoto ambao tunalea bila usaidizi wa waume na ni lazima tungejipanga jinsi ya kusaidiana kama waliounganishwa na riziki moja,” asema Bi Mary Nyambura, mshirikishi wao.

Mji huu hufurika watu kwa kuwa uko katika mpaka wa Kaunti za Embu, Kirinyaga, Machakos na Murang’a na biashara za udalali wa mavuno ya mashambani, mawe ya ujenzi, na miraa. Usisahau bidhaa na huduma za ukora.

Ni katika harakati za kujifahamisha na matukio ya mji huu ambapo Taifa Leo ilijionea genge la vijana ambao hushiriki biashara ya ‘kukamua’ mafuta kutoka kwa magari ya uchukuzi na kisha kuyauza kwa madalali ambao nao huyauza kwa raia.

Mirija ya kutoa mafuta kutoka kwa lori la Brookside eneo la Makutano, Mbeere Kusini. PICHA | MWANGI MUIRURI

Mwandishi huyu alikumbana na baadhi yao wakiiba mafuta ya lori lililokuwa limeegeshwa nje ya baa iliyoko eneo la Moska. Lori hilo lilikuwa la uchukuzi wa maziwa ya kampuni ya Brookside ambayo humilikiwa na familia ya Rais Uhuru Kenyatta.

Pia, katika eneo lilo hilo la Moska Taifa Leo ilikumbana na vijana wakipakia chang’aa kwa vijichupa. Kisha baadaye pombe hiyo ikapakiwa kwa gari dogo na kusafirishwa ili kuuzwa katika vijiji vya kaunti zilizo karibu.

Vijana katika mji wa Makutano wakipakia pombe haramu katika gari. PICHA | MWANGI MUIRURI

Aidha, Taifa Leo ilikumbana na genge lingine ambalo hushiriki biashara ya usambazaji bhangi ambayo hushukishwa katika mji huo na magari ya uchukuzi yanayohudumu kutoka Kaunti za Kaskazini Mashariki mwa nchi kupitia eneo hilo yakielekea miji ya Thika na Nairobi.

Biashara nyingine ambayo Taifa Leo ilikumbana nayo ni ile ya usafirishaji wa maharamia kutoka nchi za Ethiopia na Somalia na ambapo madalali wa kuishirikisha ni baadhi ya maafisa wa vitengo vya usalama, wafanyabiashara na raia.

“Ni biashara ambayo huwa na awamu tatu. Kuna wale madalali ambao huwafikisha maharamia hao hadi mji wa Makutano ambapo hujificha ama katika lojing’i au katika maboma ya watu binafsi wakingojea washirikishi wa mtandao huo katika mji wa Thika waje wawachukue na ambapo huwakabidhi kwa wengine ambao huwapenyeza hadi jiji la Nairobi. Wakiwa katika jiji kuu, wao huandaliwa stakabadhi za kuwapa uraia wa nchi,” afisa mmoja wa Shirika la Ujasusi (NIS) nchini akafichulia Taifa Leo.

Mnamo Januari 25, afisa wa jeshi aliyetambulika kama Frankline Muthee Gitonga alihusika katika ajali katika barabara karibu na mji huo wa Makutano akisafirisha maharamia saba kutoka taifa la Ethiopia.

Afisa huyo aliaga dunia katika ajali hiyo kabla ya wiki moja baadaye, afisa mwingine aliyetambuliwa kama Kenneth Muraga Mbua kunaswa akisafirisha maharamia wengine sita kutoka taifa lilo hilo akiwapeleka mjini Thika.

“Maharamia hao wote walinaswa na tukawafikisha kortini ambapo baada ya kuwashtaki kuwa nchini kimagendo, walifungwa kifungo cha mwezi mmoja gerezani na ilani ikatolewa kuwa wakishakamilisha kifungo hicho, watimuliwe nchini,” akasema Kamanda wa Polisi wa Murang’a Kusini Bw Alexander Shikondi.

Idara ya Jeshi ilimzika afisa huyo wao kishujaa na ambapo risasi 21 zilifyatuliwa angani kwa heshima ya kumuaga katika maziko hayo yaliyoandaliwa katika kijiji cha Kibiliaku kilichoko Kaunti ya Meru. Hii ni licha ya kuwa maafisa wa polisi waliandaa ripoti ya kuonyesha kwamba afisa huyo aliaga dunia akisambaratisha usalama.

Bw Shikondi anasema kuwa bangi ya mji wa Makutano inatatiza usalama kati mwa mji huo na ule wa Kenol na maafisa wamekuwa wakiinasa ikiwa imepakiwa kwa uchukuzi wa bodaboda, uchukuzi wa umma na ule wa mizigo.

Na sio eti serikali kuu huwa haina habari kuhusu uhalifu huo unaondelezwa katika mji wa Makutano.

Katika tarehe kadhaa za miezi miwili iliyopita, Taifa Leo ilionyeshwa nakala za ujasusi ambazo zimenakili matukio hayo yote, ikiwemo hali ya maafisa wa kituo cha polisi cha Makutano kunaswa wakiiba mahindi ya msaada wa raia walio na njaa yaliyokuwa yakisafirishwa hadi eneo la Mavuria.

Maafisa wa polisi huonekana waziwazi wakishiriki michezo ya kamari katika mji huo wa Makutano.

Matukio ya ukora huo wote yamenakiliwa chini ya jumbe EMB0741237, EMB0741237, EMB5192632, EMB8849793, EMB3245574 na EMB4879251.

Jumbe hizi husambazwa kwa makao makuu ya usalama wa nchi na pia wakuu wote wa vitengo vya usalama Kaunti ya Embu.

“Ndio, tumekuwa tukipata habari hizo za ujasusi na kwa sasa tunaandaa mikakati ya kutekeleza operesheni ya kuvunja mitandao hiyo ya ukora. Naomba tu subira na mtatuona tukiwajibikia suala hilo,” Kamanda wa Polisi wa Mbeere Kusini Bw Gregory Mutiso aliambia Taifa Leo.

Lakini kukawia kwa maafisa hao kumekera sana wenyeji.

“Sisi tumechoka na ahadi hizo za maafisa wa polisi ambao ni wazi kwamba wanakinga ukora huu,” akasema mkazi mmoja huku wengine wakiambia Taifa Leo kwamba ni kweli wamekereka.

Walisema wamechoka kuishi maisha yanayowaangazia “kama Jehanamu ndogo huku tukiambiwa hata na Rais Kenyatta mwenyewe kuwa usalama huanza na sisi raia ilhali matukio hapa yanatuonyesha waziwazi kwamba utovu wa usalama huanza na vitengo vya usalama.”

[email protected]

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Trending