Sokomoko bungeni Gedi akieleza madai ya jinsi Ruto hunyakua ardhi
Na CHARLES WASONGA
SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi Alhamisi, Aprili 14, 2022 alilazimika kuahirisha vikao vya bunge baada ya Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino kukaidi amri yake ya kumtaka aondoke bungeni kwa utovu wa nidhamu.
Spika Muturi alitoa amri hiyo baada ya Bw Owino kumrushia matusi wakati ambapo Mbunge Mwakilishi wa Wajir Fatuma Gedi alikuwa akiwasilisha stakabadhi kuhimili madai yake kwamba Naibu Rais William Ruto ni mnyakuzi wa ardhi.
Mnamo Alhamisi, Apirili 7, 2022 Bi Gedi alidai kuwa Dkt Ruto alinyakua ardhi katika eneo la Lang’ata, Kaunti ya Narok na Kaunti ya Uasin Gishu.
Kwa hivyo, Mbunge huyo alidai kuwa Dkt Ruto hana maadili stahiki ya kumwezesha kuhuDUmu kama Rais wa tano wa Kenya.
Hapo ndipo Spika Muturi alimwamuru Bi Gedi kuwasilisha ushahidi wa kuhimili madai yake. Hii ni baada ya madai hayo kuibua cheche bungeni huku wabunge wa mrengo wa muungano wa Kenya Kwanza wakimkaripia Bi Gedi kwa “kutumia jukwaa la bunge kumharibia jina Naibu Rais.”
Miongoni mwa wabunge waliokabili Bi Gedi kwa maneno makali ni pamoja na Aden Duale (Garissa Mjini), Kimani Ichung’wa (Kikuyu) na Alice Wahome (Kandara).
Bi Gedi aliingia bungeni na mkoba ambao ulikuwa umejaa stakabadhi na akapewa nafasi kuziwasilisha rasmi.
Lakini alipokuwa akifanya hivyo taharuki ilitanda bungeni huku wabunge wa mirengo miwili wakipiga kelele.
Bi Fatuma alisisitiza kuwa sharti apewe muda wa kufafanua yaliyomo katika stakabadhi hizo kabla ya kuziwasilisha rasmi.
Lakini Spika Muturi akimtaka kuziwasilisha bila kujadili masuala yaliyomo kwenye stakabadhi.
“Tafadhali Bw Spika, usiniharakishe. Sharti nielezea yaliyomo katika stakabadhi hizo kabla ya kuziwasilisha,” akasema huku Spika Muturi akionekana kukerwa.
Hapo ndipo Bw Owino alinyanyuka na kumrushia Muturi matusi makali ambayo yalimkera ndipo akaamuru aondoke
“Mheshimiwa Babu Owino nakuamuru uondoke ukumbini. Tunahitaji mjadala komavu hapa. Ondoka! Ondoka!. Walinzi, hakikisheni kwamba Babu Owino ameondoka,” Spika Muturi akafoka.
Lakini Mbunge huyo wa Embakasi Mashariki alikataa kuondoka licha ya walinzi wa bunge kumhimiza atii agizo la Spika.
Baada ya mvutano uliodumu kwa karibu dakika 30, Spika Muturi alinyanyuka na kuahirisha kikao cha bunge kabla ya shughuli muda rasmi kukamilika.
“Waheshimiwa wabunge, sheria ya bunge nambari 112 inasema hivi: Kwamba endapo fujo zitashamiri bungeni Spika ataahirisha kikao cha bunge kwa muda ambayo yeye mwenye ataweka,” akasema Bw Muturi.
Spika aliahirisha vikao vya Bunge hadi Jumanne Mei 10, 2022 saa nane na nusu alasiri.
Bunge litaendesha shughuli zake hadi Juni 9, 2022 kabla ya wabunge kupewa muda wa kuendesha kampeni kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.
Next article
Vilio, ngumi na hasira UDA ikiandaa mchujo