Sonko ajitetea kwa kupigwa marufuku na Amerika
NA CHARLES WASONGA
ALIYEKUWA gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko amejitetea vikali saa chacha baada ya kuzimwa kuzuru Amerika kutokana na tuhuma za ufisadi zinazomkabili.
Kwenye taarifa aliyotuma kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii Jumanne, Machi 8, 2022 Bw Sonko alipuuzilia mbali madai hayo akisema japo kuna kesi za ufisadi zinazomkabili kortini hajapatikana na hatia.
“Sijapatikana na hatia kuhusiana na mashtaka ya ufisadi yanayonikabili kortini kwa sababu kesi inayonikabili mahakamani haijasikilizwa na kuamuliwa. Hii ina maana kuwa sijapatikana na hatia yoyote,” akasema.
Bw Sonko alisema ni magavana wawili pekee nchini ambao “wameshtakiwa kortini kwa kutoa zabuni kwa wake na watoto wao na sio mimi.”
“Hakuna mtu wa familia yangu amewahi kupewa zabuni na serikali ya kaunti ya Nairobi nilipokuwa nikihudumu kama gavana. Huu ni ukweli unaojulikana. Mke wangu na watoto hawajawahi kuuzia serikali ya kaunti ya Nairobi vijiko au karatasi shashi, moja kwa moja au kupitia marafiki wao,” gavana huyo wa zamani akasema.
Mnamo Jumanne, Machi 8, 2022 Amerika ilimzima Sonko kuzuru nchini kwa misingi kuwa alishiriki “vitendo vikubwa vya ufisadi” alipokuwa akihudumu kama gavana.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni Anthony Blinken alisema Sonko na familia yake hawataruhusiwa kutia guu nchini humo kuanzia siku hiyo.
Hii ina maana kuwa mkewe Primrose na mabinti zake Saumu na Salma hawataruhusiwa kuzuru taifa hilo lenye uwezo mkubwa duniani kwa shughuli zozote zile.
“Amerika ina habari za kuaminika kuwa Sonko alihusika katika ufisadi alipokuwa akihudumu kama gavana wa Nairobi,” wizara hiyo ilisema kwenye taarifa Jumanne.
“Kwa hivyo, wizara inaelezea haja ya kuwepo kwa uwazi na uwajibikaji nchini Kenya,” akaongeza Eric Watnik, afisa anayesimamia masuala ya Kidiplomasia katika ubalozi wa Amerika jijini Nairobi.
Wizara hiyo ilisema kuwa sakata za ufisadi ambazo Sonko alishiriki zilihusisha utoaji rushwa na utoaji zabuni za mabilioni ya fedha bila kufuata sheria, kwa manufaa yake.
Bw Sonko aling’olewa mamlakani mnamo Desemba 2020 baada ya kuhudumu kwa miaka mitatu. Mnamo Januari 25, 2020, Rais Uhuru Kenyatta aliingilia kati usimamizi wa shughuli za serikali ya kaunti ya Nairobi kwa kubuni Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) kusimamia majukumu manne makuu ya serikali hiyo.
Luteni Jenerali Mohammed Badi aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara hiyo ambayo imepigwa vita ikidaiwa ilibuniwa kinyume cha sheria.