Sura Mpya Old Town kiti cha MCA yawapa wakazi matumaini
NA FARHIYA HUSSEIN
BAADHI ya wakazi wa Old Town katika kaunti ya Mombasa, wameelezea matumaini yao kufuatia ushindi wa kiongozi mpya katika uteuzi wa Chama cha ODM.
Bw Abdirahman Abdulkadir Hussein alishinda tikiti ya chama kwa nafasi ya MCA kwa wadi ya Old Town, na kumpindua mwakilishi wa sasa wa wadi, Bw Murfad Abdalla Amur ambaye alihudumu wadhifa huo kwa miaka 15.
Aliibuka mshindi kwa kupata kura 518 huku Bw Amur akiibuka wa pili kwa kura 58.Wakazi hao wamebaini kuwa wana matumaini ya kuona mabadiliko ndiyo maana waliipigia kura ‘sura hiyo mpya’.
Akizungumza na Taifa Leo, Bi Hilal Abdalla alisema hali ya Old Town imekuwa haibadiliki kwa miaka 10.
“Eneo hili linajulikana kwa tatizo la majitaka na magenge ya vijana. Ni wakati wa kubadilisha huo simulizi. Tuko tayari kujaribu. Watu wanasema yeye (Hussein) ni mtu wa nje, lakini sisi kama wafanyabiashara ametatua matatizo kadhaa ikilinganishwa na MCA ambaye yuko ofisini,” akasema Bi Abdalla, mkazi.
Bw Hajj Salim amemtaja Bw Hussein kama kiongozi mwenye matumaini.
“Huyu kijana amefanya mengi kwa jamii ya Old Town, amefungua biashara ndogondogo kwa vijana, akawasajili wengine kwenye masomo ya kompyuta na saluni,”alisema Bw Salim, mkazi mwingine.
Bw Hussein ambaye aametaja huu kuwa mara yake ya kwanza katika siasa za uchaguzi anasema haijakuwa rahisi kuuza ajenda zake kwa jamii ya Old Town kwani wengi walimwona kama mtu wa nje.
“Sikuzaliwa wala kukulia Mombasa. Lakini kwa muda mfupi ambao nimejichanganya na wafanyabiashara wa Old Town nilibaini wanahitaji mabadiliko,” alisema.
Ajenda yake ni ‘Anza Fresh’, ambayo yanatafsiri kwa urahisi kuwa kuanza upya, na anatumai kuwavutia wapiga kura kwa wimbi jipya la mabadiliko katika Old Town kabla ya uchaguzi wa Agosti 9.
“Wakati wa kirusi cha corona mwaka wa 2020, jumuiya ya wafanyabiashara ilijaribu kujadiliana na MCA aliyeko ili kuwaondolea kibali cha biashara kufuatia ukosefu wa biashara. Hata hivyo, mahangaiko yao yalifumbiwa macho. Sikuwa kwenye mazungumzo lakini nilihisi kitu ambacho kilichangia mimi kuwania nafasi hii. Nilikuwa nimeteua jina la mtu mwingine lakini waliamua kunichagua,” akasema Bw Hussein.
Alizaliwa katika Kaunti ya Turkana kabla ya kuhudhuria shule yake ya upili huko Kitale, kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 32 anasema kisha aliendelea na Chuo Kikuu cha Maseno na baadaye Chuo Kikuu cha Nairobi ambako alifuzu na Shahada wa Biashara.
“Ajenda yangu ni kusikiliza zaidi mahitaji ya vijana. Ukiuliza, utaambiwa mji wa Old Town inajulikana kwa shida ya magenge. Kama kiongozi ninapanga kuwashirikisha vijana katika biashara za maana ili kuwafanya wawe na shughuli,” akasema Bw Hussein.
Katibu huyo Mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara wa Soko la Marikiti anasema alichagua kujiunga na ODM kama chombo chake cha kisiasa kwa vile anaamini katika manifesto ya chama.
“Ikiwa mimi ni mwanachama wa chama tawala, itakuwa rahisi kwangu kufanya mazungumzo kwa ajili ya watu wangu,” alisema.
Nafasi ya MCA ya Old Town ilivutia wagombeaji sita ambao walikuwa wakichuana kupitia chama cha ODM, Bw Hussein, Bw Amur (MCA wa sasa), Salim Hashim, Saddam Haytham, Al-Amin Ahmed na Mohammed Hatimy.Anaongeza kuwa lengo lake kuu akishachaguliwa litakuwa kukomesha magenge na tishio la maji taka katika kata hiyo.