Tumewaua wanajeshi 17,200 wa Urusi – Ukraine
NA MASHIRIKA
KYIV, UKRAINE
JESHI la Ukraine limedai kwamba limeua wanajeshi 17,200 wa Urusi tangu kuanza kwa mapigano hayo mwezi uliopita huku mazungumzo yanayolenga kuleta amani yakitatizika baada ya washiriki kupewa sumu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la Ukraine, wanajeshi wa Urusi wamepoteza vifaru 597, magari ya kivita 1,710, ndege 127, helikopta 129 na meli saba za kivita.
Serikali ya Ukraine jana ilisema kuwa wanajeshi wake wamefaulu kudhibiti tena miji ya Donetsk na Luhansk kutoka mikononi mwa majeshi ya Urusi.Tume ya haki za kibinadamu ya Ukraine inasema kuwa jumla ya watoto 144 wameuawa katika mapigano hayo.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa watu milioni 1.8 wametoroka Ukraine na kuhamia nchi jirani na wengine milioni 2.5 wanaishi katika kambi za wakimbizi wa ndani.Hayo yanajiri huku mazungumzo baina ya Urusi na Ukraine yaking’oa nanga jijini Istanbul, Uturuki.
Shirika la habari la serikali ya Ukraine, Ukrinform, jana lilisema kuwa mazungumzo hayo yanaongozwa na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.
Mazungumzo hayo ya Uturuki yanafuatia siku chache baada ya kikosi kingine cha kufanya mazungumzo mjini Kyiv, Ukraine, kudaiwa kupewa sumu.Miongoni mwa walioathiriwa kwa sumu ni bwanyenye wa Urusi Roman Abramovich ambaye pia ni mmiliki wa klabu ya Chelsea ya Uingereza, pamoja na wawakilishi wa Ukraine.
Bwanyenye huyo ambaye amewekewa vikwazo vya kibiashara na mataifa ya Magharibi kwa kuwa mwandani wa Rais wa Urusi Vladimir Putin, amekuwa akijaribu kushiriki mazungumzo kwa lengo la kumaliza mapigano nchini Ukraine.
Baada ya mazungumzo macho ya Abramovich na wawakilishi wawili wa serikali ya Ukraine yalianza kuwa mekundu, machozi yaliwalengalenga na ngozi yao ya mikono na usoni ilichubuka.
Wataalamu wanasema kuwa sumu hiyo ambayo lengo lake halikuwa kuua, huenda ilitolewa na raia wa Urusi wenye msimamo mkali wanaounga mkono nchi yao kuvamia Ukraine.
Abramovich ni miongoni mwa wawakilishi wa Urusi ambao wako nchini Uturuki kufanya mazungumzo baada ya kutibiwa.
Bwanyenye huyo alionekana kwenye runinga ya Uturuki akiwa amevaa vifaa masikioni huku akiwa kwenye mkutano.Urusi inasema kuwa Abramovich ana uzoefu katika masuala ya upatanishi.
Jana, waziri wa mashauri ya kigeni wa Ukraine, Dmytro Kuleba, alisema kuwa wawakilishi wake wamekatazwa kula au kunywa kitu ukumbi wa mazungumzo kuepuka kupewa sumu tena.
Wakati huo huo, ripoti za kijasusi za Amerika jana zilisema kuwa Urusi ingali na azma ya kutaka kuteka nyara mji wa Kyiv.
Urusi imeshikilia kuwa haina lengo la kuteka nyara Kiev na badala yake itaelekeza nguvu zake mashariki.Kwingineko, Rais wa Amerika Joe Biden amekataa kuomba msamaha kuhusu kauli yake iliyoashiria kuwa alihimiza kubanduliwa mamlakani kwa kiongozi wa Urusi Rais Putin.
“Watu kama hao si wa kuongoza nchi, lakini wanaongoza. Licha ya kuwa ni viongozi haimanishi kuwa siwezi kuelezea hasira yangu kuhusu hilo”, Biden alisema. waandishi wa habari Jumatatu kwenye White House.