Connect with us

General News

Tuwazie kuwapunguzia mzigo hawa wawaniaji huru – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Tuwazie kuwapunguzia mzigo hawa wawaniaji huru – Taifa Leo

TAHARIRI: Tuwazie kuwapunguzia mzigo hawa wawaniaji huru

NA MHARIRI

IDADI ya Wakenya walionuia kuwania viti mbalimbali bila kutegemea vyama, inaendelea kupungua kadri na jinsi Uchaguzi Mkuu unavyozidi kukaribia.

Maelfu ya wananchi walikuwa wameazimia kuwa wawaniaji huru wa viti mbalimbali katika uchaguzi wa Agosti kwa sababu tofauti.

Mojawapo ya sababu kuu ilikuwa kwamba, waliona ingelikuwa vigumu kwao kupenya katika vyama vya kisiasa ambapo vingi hulaumiwa kwa kukosa uwazi kuhusu mbinu za uteuzi wa wagombeaji.

Uwepo wa nafasi ya raia kuwania viti bila kutegemea vyama hutoa nafasi bora kwa viongozi wema kuibuka hata wanaposhindwa kuafikia vigezo vigumu vinavyowekwa na vyama vya kisiasa.

Baadhi ya vigezo ambavyo vyama hutumia kupeana tikiti, kama vile uaminifu kwa chama cha kisiasa na kinara wake, wakati mwingi huishia tu kutoa nafasi kwa viongozi duni kupumbaza raia hadi wachaguliwe mamlakani.

Ijapokuwa kuna umuhimu wa nchi ya kidemokrasia kukuza kuwepo kwa vyama vingi vya kisiasa, inafaa wadau wanaohusika katika masuala ya uchaguzi wakumbuke kuwa sheria inaporuhusu kuwepo kwa wawaniaji huru, wanastahili kupewa nafasi ya kushindana na wawaniaji wengine wote kwa njia ya haki.

Hii ni kumaanisha, si haki kuwa na sheria zinazohitaji wawaniaji huru kutimiza vigezo sawa na vile vilivyowekewa wawaniaji ambao wanafadhiliwa na vyama vya kisiasa au vinavyokaribiana sana.

Itakuwa vyema ikiwa wadau wanaohusika katika masuala ya kubuni sheria za uchaguzi na wale wanaozitekeleza, watatafuta njia ya kulegeza baadhi ya masharti yanayowekewa wawaniaji huru.

Hii si kusema kuwe na sheria na sera zitakazoleta uhuru utakaofanya kuwe na wawaniaji tele wa kimzaha, bali vigezo vizingatie kwamba wawaniaji huru hawana viwango sawa vya ufadhili kama wenzao wanaowania kupitia kwa vyama vya kisiasa.

Mikakati itakayowekwa isitazamie kuwapendelea wawaniaji huru, bali kusawazisha uwezo kati yao na wawaniaji wanaotegemea vyama ili ushindani uwe wa haki kwao wote.

Vyama vingi vya kisiasa vimethibitishwa kukosa uhuru na haki katika uteuzi wa wawaniaji viti uchaguzini, na hivyo basi haifai tuendelee kuona nafasi pekee iliyobaki kwa wenye azma ya uongozi ikikumbwa na vikwazo vingine chungu nzima.

Ingawa muda umeyoyoma kwa suala hili kuangaziwa kabla uchaguzi wa Agosti ufike, haya ni baadhi ya masuala ambayo yanahitaji kuzingatiwa wakati tutakapokuwa tukijiandaa kwa chaguzi za miaka ya usoni.