UDA kuandaa kongamano la kitaifa la wajumbe Machi 15
Na CHARLES WASONGA
CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kimetangaza kuwa kitafanya Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wake (NDC) mnamo Jumanne, Machi 15, 2022 katika uwanja wa Michezo wa Kasarani, Nairobi.
Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Jumatatu, Februari 21, 2022, chama hicho kilisema kuwa ajenda ya mkutano huo ni kujadili sera za chama hicho, kuteua mgombea wake wa urais na kujadili masuala mengine ya UDA.
“Kulingana kipengele cha 6 (2) (iv), kipengele 31.1 (i) na kipengele 31.2 cha Katiba ya UDA, Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa UDA litafanyika mnamo Jumanne, Machi 15, 2022 katika uwanja wa Kasarani, Nairobi kuanzia saa nne asubuhi,” ikasema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Katibu Mkuu wa chama hicho Veronica Maina.
Duru ziliambia Taifa Leo kwamba kufikia Jumapili, Februari 20, 2022 hakuna watu wengine ambao walikuwa wamewasilisha maombi ya kutaka wateuliwe kuwa wagombeaji urais kwa tiketi ya UDA.
Hii ina maana kuwa Naibu Rais Dkt William Ruto ndiye ataidhinishwa na zaidi ya wajumbe 3,000 wa chama hicho kuwa mpeperushaji bendera yake katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9.
Haya yanajiri huku Msajili wa Vyama vya Kisiasa nchini Anne Nderitu kutangaza kuwa vyama vyote vya kisiasa vitahitajika kufanya makongamano yao kabla ya tarehe ya mwisho ya kura za mchujo ambayo ni Aprili 22, 2022.
“Makongamano ya kitaifa ya wajumbe wa vyama (NDCs) yanafaa kufanyika kulingana na katiba za vyama hivyo kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi zilizochapishwa katika gazeti rasmi la serikali. Hata hivyo, NDC hizo sharti zifanyike kabla ya tarehe ya mwisho ya kura za mchujo ambayo ni Aprili 22, 2022,” akasema Bi Nderitu.
Next article
Ngirita azuiliwa baada ya mdhamini wake kujiondoa