Connect with us

General News

UhuRuto wachoma mabilioni ya miradi – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

UhuRuto wachoma mabilioni ya miradi – Taifa Leo

UhuRuto wachoma mabilioni ya miradi

NA PETER MBURU

BUNGE limemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuwajibikia mabilioni ya pesa ambayo yametumbukizwa katika miradi ya Ajenda Nne Kuu, baada ya kuibuka kuwa miradi hiyo haijatimiza malengo waliyoahidiwa Wakenya, ilipozinduliwa mwaka wa 2018.

Ripoti ya Bunge baada ya kukagua nakala ya sera za serikali katika bajeti ya 2022/23 (BPS) inaonyesha kuwa miradi hiyo ya serikali ya Jubilee imefeli kwa kila hali, na sasa wabunge wanaitaka serikali kueleza jinsi ilivyotumia pesa, kabla ya kuondoka mamlakani baadaye mwaka huu.

Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti (BAC) imependekeza Wizara ya Fedha iwasilishe ripoti kuhusu kiwango cha utekelezaji wa miradi hiyo, mafanikio yake, miradi ambayo haijatimiza, thamani ya pesa zilizotumika kwa wananchi na mipango ya kuikwamua kutoka pale ilipo sasa, kufikia Machi 31.

“Ripoti hiyo iangazie habari kuhusu hatua muhimu zilizotimizwa, malengo ambayo hayajatimizwa na orodha ya miradi ya maendeleo iliyopangwa kukamilishwa mwaka 2022/23,” ripoti ya kamati hiyo ikasema.

Miradi ya Ajenda Nne Kuu inahusu miradi katika sekta nne- Afya, Kilimo, Viwanda na Ujenzi wa nyumba – ambayo Rais Uhuru Kenyatta aliamua kuelekeza rasilimali nyingi za serikali, zikiwemo mabilioni ya pesa kutoka 2018 baada ya kuchaguliwa kwa hatamu ya pili, na ambapo serikali imekuwa ikijigamba kuweka pesa kuboresha uchumi.

Hatua hiyo ya bunge ilifikiwa baada ya kamati hiyo kubaini kuwa serikali ya Rais Kenyatta haijatimiza hata lengo moja, kwa yale iliyowaahidi Wakenya, licha ya mabilioni ya pesa ambayo yametumika.

“Japo kumekuwa na maendeleo mengi katika utekelezaji, mapengo makubwa bado yanashuhudiwa. Kwa kweli, katika nguzo hizo zote nne, kuna pengo kuhusu utimizaji wake,” kamati hiyo ikasema.

Katika sekta ya viwanda ambapo serikali iliahidi kuipanua hadi ichangie asilimia 15 kwenye utajiri wa taifa (GDP) kufikia mwaka huu kutoka asilimia 9.2 mnamo 2018, kamati hiyo ilibaini kuwa hali imezorota na sekta hiyo sasa inachangia asilimia 7.6 ya utajiri wa taifa tu.

Sekta ya viwanda nchini imekuwa ikilalamika kuwa bidhaa za Kenya zinakosa ushindani kutokana na bei ya juu ya mafuta, umeme na ushuru wa juu, ambavyo vinafanya bei za bidhaa kwenda juu zaidi, ikilinganishwa na mataifa jirani. Mwaka jana, katibu wa Wizara ya Kawi, Gordon Kihalangwa, alieleza wabunge kuwa kampuni ya Kenya Power imekuwa ikipoteza Sh50 bilioni kila mwaka, kutokana na ufisadi ndani yake.

Vilevile, Mkaguzi wa Hesabu za serikali mwaka jana aliripoti kuwa kampuni ya uzalishaji kawi ya KenGen ilikuwa na miradi ya zaidi ya gharama ya Sh84 bilioni, ambayo haina matunda yoyote kwa Wakenya kwani haileti pesa jinsi ilivyotarajiwa.

Kamati hiyo pia ilibaini kuwa japo Jubilee iliahidi Wakenya kuwa wangekuwa na chakula cha kutosha kwa kuwekeza mabilioni katika kilimo cha unyunyuzaji maji na kuinua shughuli za wakulima wadogo, kwa sasa zaidi ya Wakenya milioni mbili katika zaidi ya kaunti 20 wanakumbwa na njaa.

“Athari za ukame mwaka wa 2022 ni mbaya jinsi tu ilivyokuwa kabla ya utekelezaji wa Ajenda 4,” kamati ikasema.

Ahadi ya kuongeza asilimia 34 ya mapato kwa wakulima pia bado haijatimia, kwani ripoti kadhaa, ikiwemo za serikali, zimeonyesha wakulima wadogo wanazidi kutumbukia katika umaskini nchini

Hii ni licha ya miradi mikubwa ambayo serikali ya Jubilee imetumbukiza mabilioni ya pesa bila matunda yoyote kwa Wakenya, kama ujenzi wa mabwawa ya Itare, Arror na Kimwarer ambayo kwa jumla yaligharimu zaidi ya Sh100 billioni na mradi wa Galana Kulalu uliogharimu zaidi ya Sh7 bilioni.

Katika ahadi ya kuwapa Wakenya nyumba 500,000 za bei nafuu kufikia mwaka huu, kamati hiyo ilibaini kuwa ni nyumba 1,370 pekee ambazo zimejengwa.

Katika sekta ya afya ambapo serikali iliahidi kuwalinda Wakenya wote kiafya chini ya mpango wa Afya kwa Wote (UHC) kufikia 2022, bunge lilibaini kuwa ni Wakenya milioni tatu pekee waliokuwa wamesajiliwa.

chini ya mpango huo kufikia mwaka jana, kamati hiyo ikitaja hali ya kukosa kuinua vituo vya afya kama changamoto kuu.

Kinaya ni kuwa Wakenya walipoteza zaidi ya Sh2.3 bilioni kutokana na ufisadi katika Mamlaka ya Usambazaji wa Vifaa vya afya (Kemsa) wakati wa janga la Covid-19, huku sakata ya serikali kuu kulazimisha zile za kaunti kununua vifaa vya afya ambavyo nyingi hazikuhitaji (MES), ikihofiwa kusababisha hasara kubwa. Vifaa hivyo viligharimu jumla ya Sh63 bilioni na hadi sasa kuna kaunti ambazo hazijawahi kuvitumia, vikizidi kuharibika.

Wabunge wanaitaka wizara ya afya kuwasilisha ripoti kuhusu mpango huo wa vifaa vya afya kwa kaunti, ikieleza mafanikio yake, changamoto na thamani ya pesa. “Ni muhimu kuwa masuala muhimu yanayozingira mpango huu yaangaziwe ili kuhakikisha upokezanaji mwema.”

Mnamo 2019, ilibainika kuwa Hazina ya Afya Kitaifa (NHIF) ilikuwa imepoteza Sh10 bilioni kutokana na kulipa hospitali kwa huduma ambazo hazikutolewa.