[ad_1]
KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Unapokuwa kwenye mapumziko usikae bure, zoea kupumzika na kazi
NA WALLAH BIN WALLAH
BINADAMU anaweza kuacha kufanya shughuli zake kwa kisingizio kwamba ati anapumzika!
Anaweza kuacha kabisa kuyatekeleza majukumu yake muhimu kwamba yuko mapumzikoni au likizoni!
Lakini anapokaa bure hivyo ajue kwamba muda unayoyoma tu! Wakati haumsubiri mtu yeyote awaye tajiri, maskini, mkubwa wala mdogo! Wakati haumngojei hata mfalme!
Kwa mintarafu ya utangulizi huo, ninakushauri kwamba ukitaka kufanikiwa katika maisha, usikae bure! Enda na wakati ufanye chochote unachoweza bila kungojea kesho au baadaye! Mafanikio ya maisha hayana urafiki na watu wazembe wanaoketi bila kujishughulisha kutekeleza wajibu! Ajizi ajizi ni nyumba ya njaa! Wakati ni upepo ukipita haurudi! Tumia wakati vizuri!
Fanya kazi zako na shughuli zako wakati wowote unapopata nafasi. Ukichelewa ama ukiacha kutimiza wajibu wako leo utapitwa na wakati ubakie hapo bila kufanikiwa maishani! Halafu utamlaumu nani? Utamlilia nani? Litakuwa kosa la nani?
Ndugu wapenzi, mwanadamu ana majukumu mengi ya kutekeleza hapa duniani ili ajitafutie riZiki na mahitaji muhimu kujikimu! Tusidanganyike kwamba kuna muda au nyakati za mapumziko au likizo za kukaa bure bila kufanya shughuli zozote ama kuzurura tu! Utakaaje bure bila shughuli ilhali unataka kula, kuoga, kuvaa na kuishi? Utavipataje vitu hivyo usipovifanyia kazi na kuvitafuta?
Ewe mwanafunzi uliyefanya mtihani nawe unayengojea kuendelea na masomo, hapo mapumzikoni au likizoni usikae bure! Endelea na kazi zako kidogo kidogo huku ukipumzika! Huko ndiko kupumzika na kazi! Amiin!!!!!!!!!!
Wallah Bin Wallah ni Mwandishi Mlezi wa Kiswahili na Mkurugenzi wa WASTA KITUO CHA KISWAHILI kilichoko Ngong Matasia Nairobi Kenya.
[email protected]
[ad_2]
Source link