Urusi yatishia kuzusha Vita vya Tatu vya Dunia iwapo mataifa ya Magharibi yataendelea kupeleka silaha Ukraine
NA MASHIRIKA
MOSCOW, URUSI
URUSI imetishia kuanza vita vya dunia iwapo mataifa ya Magharibi ikiwemo Amerika, yataendelea kutoa msaada wa silaha kwa Ukraine.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Urusi, Sergey Lavrov jana alisema kuwa mataifa ya Magharibi yamekuwa yakisaidia Ukraine na kuna hatari ya kulipuka kwa Vita vya Dunia III.
Lavrov alisema Urusi huenda ikalazimika kuanza kutumia silaha za maangamizi makubwa za nyuklia ‘kujilinda’ dhidi ya mataifa ya Magharibi.
Majeshi ya Urusi Jumatatu yalianza kushambulia miundomsingi ya reli kwa lengo la kuzuia silaha kutoka mataifa ya kigeni kuingia Ukraine.
Lavrov, aliyekuwa akizungumza katika mahojiano na runinga ya serikali ya Urusi, alisema kuwa mataifa ya Magharibi yamekuwa yakipeleka silaha hatari nchini Ukraine kwa lengo la kuangamiza wanajeshi wa Urusi.
“Mataifa ya Magharibi yamekuwa yakipeleka silaha hatari kama vile roketi za kutungua makombora, magari ya kuzuia risasi, mabomu na ndege zisizo na rubani. Huo ni uchokozi na lengo lao ni kushambulia Urusi,” akasema Lavrov.
Urusi ilitoa onyo hilo huku mataifa ya Magharibi yakiahidi kutoa silaha zaidi kwa Ukraine.Amerika inatarajiwa kukutana na viongozi wa nchi 40 kujadili jinsi ya kutoa msaada wa silaha kwa Ukraine.
Mawaziri wa ulinzi wa mataifa wanachama wa Muungano wa Ulinzi wa nchi za Amerika na Ulaya (NATO) wanaendelea na mkutano nchini Ujerumani kujadili vita nchini Ukraine.
Jumatano, waziri wa ulinzi wa Uingereza, Lloyd Austin anayeongoza mkutano huo, alisema kuwa mataifa ya Ulaya yanalenga kufifisha jeshi la Urusi kiasi kwamba halitakuwa na uwezo wa kuvamia tena nchi nyingine katika siku za usoni.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guteress jana Jumanne alikutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin jijini Moscow katika juhudi za kumsihi akubali kusitisha au kumaliza kabisa uvamizi wa nchi yake dhidi ya Ukraine ambao umedumu kwa miezi miwili.
Msemaji wa Guterres alisema mkuu huyo wa UN kesho atazuru mjini Kyiv kukutana na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.
Akiwa njiani kuelekea Moscow, Guterres alikutana na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, ambaye alijaribu bila mafanikio kusihi Urusi na Ukraine kumaliza vita.
Guterres ametoa wito mara kadhaa wa kusitisha mapigano kwa ajili ya shughuli za kibinadamu au kusitisha mapigano kwa muda, lakini bila mafanikio.
Majeshi ya Urusi jana Jumanne yalijigamba kuwa yaliua wanajeshi 500 wa Ukraine usiku wa kuamkia jana Jumanne.
Wizara ya ulinzi ya Urusi ilidai kuwa iliwaua wanajeshi hao baada ya jeshi lake la anga kushambulia maeneo 87 ya kijeshi nchini Ukraine.
Maghala mawili ya silaha katika eneo la Kharkiv yalidaiwa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyoharibiwa na wanajeshi wa Urusi katika mashambulio hayo.