Ushindi dhidi ya ufisadi, Kenya ikirejeshewa Sh450 milioni kutoka Jersey
LONDON, Uingereza
Na BBC
SERIKALI ya Kenya itapokea Sh450 milioni, pesa za ufisadi ambazo zilikuwa zimefichwa katika kisiwa cha Jersey na aliyekuwa Waziri wa Fedha Chris Okemo na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampeni ya kusambaza umeme, Samuel Gichuru.
Hii ni baada ya Kenya na utawala wa Jersey, kutia saini makubaliano ambayo yatawezesha pesa hizo kurejeshwa nchini ili kutumika katika ununuzi wa vifaa vya kupambana na Covid-19. Mkataba huo ulitiwa saini Machi 28, 2022 na Mkuu wa Sheria wa Jersey na Balozi wa Kenya nchini Uingereza Manoah Esipisu.
Pesa hizo zilitwaliwa na utawala wa kisiwa hicho cha Jersey, kilichoko Uingereza, mnamo 2016, kufuatia kushtakiwa kwa kampuni ya Windward Trading Ltd kuwa makosa ya ulanguzi wa pesa. Mahakama kisiwani Jersey iliamua kuwa mali ya kampuni hiyo ambayo ilikuwa inamilikiwa na Bw Gichuru, itwaliwe. Mali ya thamani ya dola 4.9 milioni (sawa na Sh490 milioni) ilitwaliwa na utawala wa Jersey.
Inadaiwa kuwa sehemu kubwa ya pesa hizo zilitokana na sakata za ufisadi nchini Kenya kati ya 1999 na 2002, na ndio sasa zinarejeshwa. Bw Okemo alihusishwa na kesi hiyo baada ya kubainika alipokea hongo kutoka kwa kampuni kadha za kimataifa na kuwasilisha pesa hizo kwa Windward Trading Ltd iliyosajiliwa katika kisiwa cha Jersey kinachojitawala.
Pesa hizo, Sh450 milioni, zitarejeshwa Kenya chini ya Mpango wa Kurejeshwa Nchini kwa Mali inayotokana na Ufisadi (Framework for Return of Assets from Corruption and Crime in Kenya-FRACCK). FRACCK ilitiwa saini mnamo Agosti 2018 katika uwepo wa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May. Ulitiwa saini na Rais wa Uswizi Alain Berset alipozuru Kenya. Vile vile, ulitiwa saini na Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Jersey Ian Gorst alipofanya ziara rasmi nchini Kenya mnamo Desemba 2018.
FRACCK ndio iliamua kuwa pesa hizo zitakazorejeshwa Kenya zitumiwe kufadhili mipango ya kupambana na Covid-19. “Nina furaha kwamba tumekamilisha makubaliano haya kurejesha pesa hizo ili zitumiwe kupiga jeki juhudi za kupambana na Covid-19,” akasema Seneta Gorst.
“Ufisadi ni uhalifu wenye madhara makubwa mno; ya moja kwa moja na yale ambayo sio ya moja kwa moja kwa watu” akaongeza. Gorst alisema kuwa kutiwa saini kwa makubaliano ya kurejesha kwa pesa hizo Kenya kunaonyesha kuwa Jersey haivumilii ufisadi na uhalifu wa kifedha.
“Inaashiria kuwa maafisa wetu hawatasita kutwa kukabiliana na ufisadi na kuhakikisha kuwa zimerejeshwa kusaidia watu walioathiriwa na uovu huo,” akaeleza. Kwa upande wake, Balozi Esipisu alisema hatua hiyo inaonyesha kuwa Serikali ya Kenya imejitolea kupambana na aina zote za ufisadi.
“Kurejeshwa kwa Sh450 milioni kunaonyesha kuwa wafisadi hawawezi kujificha popote duniani. Sharti watapatikana,” akaeleza Bw Esipisu. Balozi huyo alikariri kuwa Kenya imejitolea kushirikiana na mataifa kama vile Uingereza, Uswizi na Jersey kufikia malengo ya mpango wa FRACCK.
“Mataifa mengine pia yanaweza kujifunza kutokana na mfano huu ili kufuatilia pesa za wizi na kuzirejesha chini ya mpango kama huu wa FRACCK,” Esipisu akaongeza.
Next article
Mwaura afungua moyo baada ya jaribio kumvua taji la useneta