OKANIWA KEN: Ushirikiano wa Kenya na Japan utaendelea kuimarika, hasa kiuchumi
NA OKANIWA KEN
MNAMO Aprili mosi, nilimkabidhi Rais Uhuru Kenyatta stakabadhi zangu za uthibitisho.
Maneno yake matamu aliponikaribisha, yalikuwa ushahidi wa urafiki wa muda mrefu kati ya nchi zetu mbili.
Japan inathamini nafasi ya Kenya kama nanga ya utulivu Afrika Mashariki.
Hivi majuzi wakufunzi wa Jeshi la Kujilinda la Japan waliendesha mafunzo ya vifaa vizito vya uhandisi kwa wanajeshi 35 kutoka Kenya, Uganda na Ghana jijini Nairobi.
Idara ya Walinzi wa Pwani ya Kenya inatumia meli 17 za doria zilizotolewa na Japan ili kudumisha utulivu baharini.
Huku Japan ikitarajia kujiunga na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama mwanachama asiye wa kudumu mwaka ujao (2023), ninatumai kuendeleza ushirikiano huo.
Mwezi Agosti, Japan itaratibu (Mkutano wa Kimataifa wa Tokyo wa Maendeleo ya Afrika) TICAD 8 nchini Tunisia.
Kama mnavyokumbuka, mkutano wa sita wa TICAD 6, wa kwanza kufanyika barani Afrika, ulifanyika Nairobi mwaka wa 2016.
Hii ni ishara ya kweli ya uaminifu wa kweli uliopo kati ya nchi zetu mbili.
Nina furaha kuwaripotia ya kwamba, tangu mwaka wa 2016, idadi ya makampuni kutoka Japan yanayofanya kazi Kenya imeongezeka maradufu hadi zaidi ya 100.
Uhusiano wetu wa kibiashara umepanuka sio tu kwa idadi, bali pia katika wigo kutoka kwa biashara hadi uzalishaji wa ndani, na uwekezaji.
Kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa TICAD 8, Japan na Kenya zitaandaa Kongamano la pamoja la Kiuchumi la Umma na Kibinafsi la Japan-Afrika Mei 3 jijini Nairobi.
Mawaziri, viongozi wa wafanyabiashara kutoka Japan na Afrika wanatarajiwa kushiriki.Mwaka wa 2023, ukiwa miaka 60 ya Uhuru wa Kenya, pia itakuwa maadimisho ya miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia wa nchi hizi mbili.
Hii ni fursa nzuri ya kusherekea mafanikio yaliyopita na kuzingatia ushirikiano wa siku zijazo. Ninatazamia kufanya kazi kwa karibu na Serikali na watu wa Kenya ili kukuza urafiki wetu zaidi.Mwandishi ni Balozi wa Japan, hapa Kenya.