Connect with us

General News

Uteuzi Ukambani sasa wamnyima Kalonzo usingizi – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Uteuzi Ukambani sasa wamnyima Kalonzo usingizi – Taifa Leo

Uteuzi Ukambani sasa wamnyima Kalonzo usingizi

NA PIUS MAUNDU

KINARA wa Wiper Kalonzo Musyoka anajikuna kichwa, siku 10 tu kabla ya chama hicho kuandaa uteuzi wake, huku wandani wake waking’ang’ania tiketi ya kuwania ugavana katika ngome ya Kitui na Machakos.

Katika gatuzi la Kitui, aliyekuwa Gavana Dkt Julius Malombe na aliyekuwa Balozi wa Kenya nchini Uganda, Bw Kiema Kilonzo wapo katika ushindani mkali ili kutwaa tiketi ya Wiper.

Mshindi kwenye mchujo huo atapambana na Gavana wa sasa Bi Charity Ngilu, pamoja na seneta wa zamani, Bw David Musila, ambaye hivi majuzi alihamia Jubilee.

Pia aliyekuwa Naibu Gavana wa Nairobi, Bw Jonathan Mueke analenga kiti hicho kupitia UDA.

Hali ni hiyo hiyo katika kaunti jirani ya Machakos, ambapo ushindani mkali unaendelea kushuhudiwa kati ya mbunge wa Mavoko, Bw Patrick Makau na aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Uchukuzi Bi Wavinya Ndeti.

Wawili hao ni wandani wa Bw Musyoka na wengi wanasubiri kuona nani atatwaa tiketi ya Wiper huku muhula wa pili wa gavana wa sasa Dkt Alfred Mutua ukielekea kutamatika.

Dkt Malombe alizindua rasmi azma yake mnamo Jumamosi mjini Kitui, ambako alishambulia uongozi wa Gavana Ngilu kwa kukosa kutimiza ahadi kadhaa ilizotoa kwa wakazi 2017.

“Tunafaa kuungana kuokoa kaunti yetu hasa kimaendeleo ili kuwanufaisha watoto wetu, wajukuu na vitukuu. Sote tunafaa kuweka juhudi kuhakikisha kuwa tunazuia kaunti yetu kuporomoka zaidi,” akasema Dkt Malombe ambaye alihudumu kama gavana wa kwanza wa kaunti hiyo kutoka 2013-2017.

Hesabu za ugavana katika kaunti hiyo zinazidi kumkosesha Bw Musyoka usingizi, hasa baada ya mwanawe Kelvin Muasya kujitosa ulingoni na kutangaza kuwa atakuwa mgombeaji mwenza wa Bw Kilonzo.

Ingawa Bw Musyoka hivi majuzi alitangaza kuwa amemruhusu mwanawe kuingia kwenye ulingo wa siasa, alimwonya kuwa amakinike kwenye safari hiyo ili asimharibie katika siasa za kitaifa.

Bw Musyoka vilevile alionya kuwa mgawanyiko unaoendelea kushuhudiwa kati ya Mabw Kilonzo, Musila na Dkt Malombe huenda ukamnufaisha Bi Ngilu na mara nyingi amewarai wakubaliane wenyewe, ili mmoja wao apambane na gavana huyo debeni.

Bw Makau naye ameapa kuwa hatamwachia Bi Ndeti tiketi ya Wiper licha ya mbunge huyo wa zamani wa Kathiani kudaiwa kupigiwa upatu na Bw Musyoka.

Bw Makau na Bi Ndeti ni jamaa lakini Bi Ndeti amekuwa akisisitiza kuwa anastahili tiketi ya Wiper, akidai alipokonywa ushindi katika uchaguzi mkuu wa 2017.

Licha ya duru kuarifu kuwa Bi Ndeti anapendelewa na Bw Musyoka, matokeo ya kura za utafiti ambazo ziliwasilishwa kwa Wiper zinaonyesha kuwa Bw Makau yupo kifua mbele katika kiny’ang’anyiro cha ugavana wa Masaku. Utafiti huo ulimpa asilimia 58 huku Bi Ndeti akiwa na asilimia 31.

Mbunge huyo jana alikariri kuwa yupo huru kugura na kuwania kama mgombeaji huru iwapo Wiper itatoa tiketi ya moja kwa moja kwa Bi Ndeti.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending