Connect with us

General News

Uteuzi wa majaji wapigwa breki – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Uteuzi wa majaji wapigwa breki – Taifa Leo

Uteuzi wa majaji wapigwa breki

NA RICHARD MUNGUTI

ZOEZI la kuwaajiri majaji 26 limeharamishwa na mahakama kuu.

Akisitisha hatua ya Tume ya Kuajiri Watumishi wa Mahakama (JSC), Jaji Antony Mrima alisema tayari kuna majaji walioteuliwa na bado hawajaapishwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Jaji Mrima alisema hakuna uhakika ikiwa majaji hao 26 wakiteuliwa wataapishwa na Rais ama watakataliwa.

Jaji Mrima alisema Jaji Mkuu (mstaafu) David Maraga aliwateua majaji 40 na majina yao kuwasilishwa kwa Rais Kenyatta, lakini akakataa majaji sita na kuwaapisha 34.

Miongoni mwa majaji waliokataliwa ni Jaji George Odunga, Aggrey Muchelule, Weldon Korir na Joel Ngugi. Wengine aliowakataa ni Judith Omange na Evans Makori.

JSC ilikuwa imeorodhesha majina ya majaji, mahakimu na mawakili zaidi ya 150 kuteua majaji 20 wa mahakama kuu na sita (6) wa mahakama ya rufaa.

Akisitisha zoezi hilo la kuwateua majaji hao Jaji Mrima alisema shughuli hiyo inakinzana na sheria.

Jaji Mrima aliamuru JSC ikome kuanza shughuli hiyo ya kuwahoji wawaniaji hadi kesi iliyowasilishwa na Katiba Institute isikilizwe na kuamuliwa.

Wakili Duddley Achiel anayewakilisha Katiba Institute alieleza Jaji Mrima kwamba kuna shauku kubwa ikiwa uteuzi wa majaji hao utakamilishwa ama utakwama njiani kama hapo awali.

Akitoa uamuzi huo Jaji Mrima alisema Katiba Institute iko na kesi iliyo na mashiko kisheria na kuamuru JSC isitishe zoezi la mahojiano hadi kesi iiliyoshtakiwa isikilizwe na kuamuliwa.

Jaji Mrima alisema kwa vile rufaa ya kushurutisha kuteuliwa kwa majaji sita waliosalia ingali inasubiri uamuzi katika mahakama ya rufaa, zoezi la kuajiri majaji wapya lahitaji kusimamishwa.

Pia alisema kuna suala la kushiriki kwa Rais katika uteuzi wa majaji ambalo halijaamuliwa.

Jaji huyo aliagiza kesi hiyo isikilizwe Julai 6, 2022.