– Paul Pogba kwa sasa anauguza majeraha ndogo kwenye uso wake baada ya kugongana na Victor Lindelof wakati wa mazoezi
– Mfaransa huyo kupitia Instagram aliwaonyesha mashabiki wake majeraha aliyoyapata huku akimpongeza Mswidi huyo kwa uledi wake kwenye safu ya ulinzi
– Nyota huyo wa zamani wa Juventus amekuwa akishirikiana vyema na Bruno Fernandes katika safu ya kati
Paul Pogba aliwachwa akiuguza majeraha baada ya kugongana na mchezaji mwenzake wa Man United, Victor Lindelof wakati wa mazoezi.
United, ambao wameandikisha matokeo bora wanapania kurejea uwanjani siku ya Jumatatu, Julai 13, wakati watakapokuwa wakigarazana na Southampton ugani Old Trafford.
Pogba kupitia Instagram aliwaonyesha mashabiki wake majeraha aliyoyapata.Picha:Getty Images. Source: Getty Images
Katika mojawapo ya picha, Pogba alionyesha jeraha ndogo kwenye mdomo wake wa juu kudhihirisha majereha aliyosababishiwa na difenda huyo Mswidi.
“Victor uliniangamiza! Angalia hii kaka . Mungu Wangu! Hii ndio hutokea ukikutana na jamaa wa barafu Victor Lindelof,” alisema Pogba.
Wakati huo huo, mshindi huyo wa Kombe la Dunia anaonekana kufurahia wakati wake Old Trafford tangu kurejea kwake baada ya misururu ya majeraha.
Amekuwa akishirikiana vyema na Bruno Fernandes katika safu ya kati na sasa anatazamia kusalia Old Trafford baada ya msimu huu.
Alikuwa amehusishwa pakubwa na kugura klabu hiyo kutokana na ugomvi dhidi ya Mashetani Wekundu huku Real Madrid na Juve vikiwa miongoni mwa vilabu vilivyokuwa vikihusishwa na uhamisho wake.