Connect with us

General News

Vilio, ngumi na hasira UDA ikiandaa mchujo – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Vilio, ngumi na hasira UDA ikiandaa mchujo – Taifa Leo

Vilio, ngumi na hasira UDA ikiandaa mchujo

NA WANDISHI WETU

UCHAGUZI wa mchujo wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Naibu Rais William Ruto, jana ulikumbwa na hitilafu tele, fujo na vilio kuhusu wizi wa kura.

Chama hicho jana kiliandaa kura za mchujo katika vituo 15,000 kwenye kaunti 36 kote nchini lakini madai ya wizi na vurugu zilitanda katika maeneo ya Bonde la Ufa na Mlima Kenya ambapo kina uungwaji mkono mkubwa.

Wanachama wa UDA katika kaunti 13 walikuwa wakichagua gavana, kaunti 18, seneta, kaunti 28 wawakilishi wa wanawake na maeneobunge 13, wabunge na wadi 834 madiwani.

Katika Kaunti ya Bomet, shughuli ya kupiga kura ilitatizika katika vituo mbalimbali kufuatia kuwepo kwa madai kwamba, baadhi ya karatasi za kura zilikuwa zimewekewa alama kupendelea baadhi ya wawaniaji.

Baadhi yao walilalama kuwa, wasimamizi wa vituo vya kupigia kura walipokea karatasi za kura Jumatano jioni na kuzipeleka majumbani mwao ambapo baadhi ya wanasiasa waliwekewa alama usiku.

Mwaniaji wa ugavana Dkt John Mosonik, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu (Knut) Wilson Sossion na mwaniaji wa ubunge wa Bomet ya Kati Joyce Korir ni miongoni mwa wanasiasa waliolalamikia kuibiwa kura katika Kaunti ya Bomet.

Dkt Mosonik anamenyana na gavana wa sasa, Hillary Barchok, kusaka tiketi ya UDA na mshindi atapambana na aliyekuwa Gavana wa Bomet, Isaac Ruto wa Chama cha Mashinani (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Bi Korir ambaye pia ni Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Bomet, Seneta Christopher Langat, Bw Sossion na Dkt Mosonik walitaka uchaguzi huo wa mchujo kuandaliwa upya.

Katika Kaunti ya Embu, kamati ya nidhamu ya UDA, imealika wanasiasa Norman Nyaga na John Muchiri kutokana na madai ya kufadhili wahuni kuteketeza masanduku ya kura baada ya kuzuia lori lililokuwa limebeba vifaa hivyo nje ya hoteli ya Izaak Walton Inn.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Paul Karuga alisema wamepokea video inayothibitisha kuwa wawili hao walihusika na uhalifu huo.

Mwaniaji wa ubunge eneobunge la Bobasi, Kaunti ya Kisii, Lucas Mogoa, alikamatwa kutokana na madai ya kuiba masanduku ya kura wakati wa mchujo wa UDA.

Mkuu wa Polisi wa eneo hilo, Kipkemoi Kipkulei alisema kuwa, mwanasiasa huyo alizuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Nyamache.

Shughuli ya kupiga kura katika kituo cha Cheptarit, eneobunge la Chesumei, Kaunti ya Nandi, ilitatizika kwa muda kufuatia vurugu zilizozuka Seneta Samson Cherargei, anayewania ugavana, alipokataa kupanga foleni na wapigakura wengine.

Bw Cherargei aliwasili kituoni akiwa ameandamana na wafuasi wake na baadhi ya wawaniaji na kulazimisha kufululiza moja kwa moja hadi chumba cha kupigia kura.

Mwaniaji wa udiwani katika eneobunge la Mathare, Nairobi, Elizabeth Waithera, 39, alijeruhiwa baada ya kushambuliwa na kundi la wahuni kura za mchujo zilipokuwa zikiendelea katika shule ya Msingi ya Kiboro.

Polisi walilazimika kuingilia kati katika Shule ya Msingi ya Kayole One, Embakasi ya Kati, baada ya wapigakura kuzua vurugu wakilalamikia kucheleweshwa kwa masanduku ya kura.

Wafuasi hao wa UDA walitishia kupiga wasimamizi wa uchaguzi kwa kujikokota.

Katika Kaunti ya Kajiado, mwaniaji wa ugavana Bi Peris Tobiko alipuuzilia mbali uchaguzi wa jana huku akisema ulikumbwa na visa vya udanganyifu.

“Nilidhani chama cha UDA kinazingatia demokrasia kumbe kina wenyewe,” akalalama mbunge huyo wa Kajiado Mashariki ambaye Oktoba mwaka jana alialika Dkt Ruto nyumbani kwake na kumchinjia ng’ombe na kusababisha mumewe, Kishanto Ole Suuji, kumripoti kwa polisi.

Katika Kaunti ya Tharaka Nithi, masanduku ya kura yaliharibiwa katika Shule ya Msingi ya Ntatua, eneobunge la Maara, na vijana waliovamia kituo hicho wakidai kuwepo njama ya wizi wa kura.

Wawaniaji wawili walijeruhiwa na mtu mmoja akakamatwa baada ya vurugu kuzuka kituoni katika Wadi ya Kimaeti, eneobunge la Bumula, Kaunti ya Bungoma.

Hali ilikuwa sawa na hiyo katika kituo cha Njoguini, Laikipia Mashariki ambapo mbunge wa eneo hilo, Amin Deddy alidai kulikuwa na karatasi za kura zilizotiwa alama usiku wa kuamkia jana.

Mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi ya UDA, Anthony Mwaura jana alisema uchaguzi ulitatizwa kwa zaidi ya masaa mawili katika eneobunge la Marakwet Mashariki baada ya majangili kuvamia kijiji na kuua mtu mmoja.

Kulingana na Bw Mwaura, uchaguzi wa UDA katika maeneo ya Turkana Mashariki, Turkana ya Kati, Nandi Hills, Narok Kusini na Nakuru Magharibi utafanyika Aprili 19.

Ripoti za Vitalis Kimutai, Mercy Chelang’at, Gitonga Marete, Alex Njeru, Ndubi Moturi, Stanley Kimuge, Tom Matoke, Florah Koech na John Njoroge.