Vituo vyafungwa tena ukosefu wa mafuta ukiendelea
NA WAANDISHI WETU
UHABA wa petroli unaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini huku baadhi ya vituo vya mafuta vikifungwa kwa kukosa bidhaa hiyo.
Wahudumu wa bodaboda na waendeshaji magari katika maeneo ya Kaskazini mwa Bonde la Ufa bado wanahangaika kwa uhaba wa petroli.
Ukosefu huo umekithiri zaidi katika Kaunti ya Uasin Gishu na nyingine jirani huku wenye vituo mbalimbali wakiamua kuvifunga.
Haya yanajiri hata baada ya serikali kuhakikishia Wakenya kuwa uhaba huo utatatuliwa.
Ripoti inaonyesha kuwa, wafanyabiashara wa magendo kwenye mpaka wa Malaba na Lwakhakha katika Kaunti ya Bungoma wanajizolea faida maradufu, kwa kuuza petroli ambayo wananunua nchi jirani.
Wamepandisha bei ya petroli ambapo wanauza lita moja Sh300.Uhaba huo bado unaendelea kushuhudiwa huku watuamiaji wakipanga foleni katika vituo mbalimbali vya petroli.
Waendeshaji magari katika miji mikuu na maeneo ya mashambani bado wanakabiliwa na uhaba mkubwa.Wafanyabishara waliozungumza na Taifa Leo mnamo Jumatatu katika maeneo ya Chwele, Webuye, Kimilili, Kapsokwony na Naitiri walisema bado hawajapata petroli ya kutosha.
Peter Karanja, mmoja wa watumiaji petroli Kaunti ya Uasin Gishu, alisema kuwa baadhi ya vituo havina petroli na hilo limefanya bei ya nauli kupanda hususan wakati huu ambapo wanafunzi wanasafiri kwenda shuleni kwa mwaka mpya wa masomo.
Kwa mfano, magari ya umma katika barabara kuu ya Eldoret-Nairobi sasa yanatoza nauli kati ya Sh1,200 na Sh1,500 kutoka Sh800 awali.
Baadhi ya vituo vilivyokuwa na mafuta Jumatatu ni Shell, Total na Hass katika eneo la Maili Nne.
“Kuna uhaba mkubwa wa petroli. Nililazimika kujaza pikipiki yangu Jumatatu asubuhi kwa Sh1,800. Hiyo itanisukuma wiki moja,” akaeleza James Njuguna ambaye ni mhudumu wa bodaboda.
Uhaba huo pia ulishuhudiwa katika Kaunti ya Marakwet ambapo wanabodaboda walishutumu serikali kwa kukoasa kusuluhusha tatizo hilo, jambo linalofanya wapate hasara kubwa.
“Serikali inafaa isuluhishe uhaba wa petroli haraka upesi. Watu wengi sana wanaumia,” akasema Bw Korat.
Kwa upande wake, Kennedy Simiyu kutoka Lodwar alisema bei ya petroli katika eneo hilo imepanda hadi Sh160 lita.Alieleza kuwa baadhi ya vituo vya mafuta vimefungwa eneo la Lodwar.
“Wahudumu wa bodaboda wamepandisha nauli. Ukitaka kufika mjini unalipa Sh50,” akasema mkazi wa eneo hilo Mike Ekono.
Wananchi mbalimbali wanazidi kulalamika huku wakitoa wito kwa serikali kutatua mgogoro huo nchini.
“Tunapata hasara nyingi. Hatuwezi kutoa huduma ikiwa kuna uhaba wa petroli,” akasema Bw Korat.
Ripoti za FRED KIBOR, STANLEY KIMUGE, BRIAN OJAMAA, OSCAR KAKAI na SAMMY LUTTA
Next article
Safari ya mwisho ya Kibaki yaanza rasmi