Connect with us

General News

Vyuo vikuu vya umma kuzidi kuumia kifedha – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Vyuo vikuu vya umma kuzidi kuumia kifedha – Taifa Leo

Vyuo vikuu vya umma kuzidi kuumia kifedha

NA FAITH NYAMAI

VYUO vikuu vya umma nchini vitaendelea kukumbwa na matatizo ya kifedha baada ya mapendekezo kwenye bajeti yao kukosa kutengewa fedha za kutosha katika bajeti iliyosomwa mnamo Alhamisi.

Waziri wa Fedha Ukur Yattani alitengea vyuo vikuu vya umma Sh91.2 bilioni kwenye bajeti hiyo japo makadirio aliyokuwa amewasilishiwa na sekta hiyo ya elimu yalikuwa Sh102.807 bilioni.

Iwapo vyuo hivyo vingetimiziwa mapendekezo yao kwenye bajeti, vingelipa madeni yote yanayodaiwa, mishahara ya wafanyakazi wao na wahadhiri pamoja na kujikimu hadi bajeti nyingine isomwe mwaka 2023.

Ingawa pesa vyuo hivyo vilitengewa zilikuwa nyingi kuliko Sh76.3 bilioni mwaka jana, vyuo vya umma sasa vimelemewa na madeni na havina fedha za kutosha kuendeleza oparesheni zao.

Wanafunzi wengi ambao wanategemea ufadhili wa HELB wamekuwa wakipitia wakati mgumu kiuchumi kwa sababu bodi hiyo haiwezi kuwatumia pesa kwa wakati kutokana na ufadhili duni.

Katika mwaka wa kifedha wa 2021/22, zaidi ya wanafunzi 75,000 walikosa ufadhili wa HELB kwa sababu Hazina ya Kifedha haikuwasilishia bodi hiyo ya elimu ya juu pesa za kutosha.

Alipowasilisha makadirio ya bajeti ya vyuo vikuu vya umma mbele ya kamati ya elimu bungeni, Katibu katika Wizara ya Elimu anayesimamia idara ya elimu ya juu Simon Nabukwesi alitaja Masinde Muliro, Nairobi, Moi, Kenyatta na Jomo Kenyatta (JKUAT) kama vyuo vikuu ambavyo vimekuwa vikipokea mgao mdogo kutoka kwa serikali.

Vyuo vikuu vingine ni Meru, Kirinyaga, Garissa navyo vilikuwa vikihitaji Sh100 milioni zaidi kulipa mishahara ya wahadhiri na wafanyakazi wao.

Chuo Kikuu cha Nairobi kinahitaji Sh112.5 milioni zaidi kulipa gharama za kesi huku chuo kikuu cha Rongo kikihitaji Sh167 milioni kujenga maktaba mpya.

Pia Chuo Kikuu cha Kiufundi Kenya (TUK) kiliomba Sh150 milioni kujaza upungufu wa fedha uliokuwa ukikikabili.

Wizara ya Elimu ilikuwa imeomba hazina kuu Sh200 milioni zaidi ili kugharimia masalio kwenye mkataba wa CBA 2017-2021 walioafikiana nao na viongozi wa miungano ya wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu.

Kwenye bajeti hiyo, Bw Yatani alitengea vyuo vya kiufundi Sh5.2 bilioni kufadhili masomo ya wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya kiufundi.