Waathiriwa wa ghasia waonya wanasiasa
NA FARHIYA HUSSEIN
WAKAZI wa eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, ambao waliathirika na ghasia wakati wa chaguzi zilizopita, wamewataka wanasiasa wakomeshwe kueneza uchochezi na chuki zinazoweza kuzamisha nchi kwa fujo mara nyingine mwaka huu.
Waathiriwa hao ambao wameungana chini ya kikundi kinachopigania haki yao kulipwa fidia kwa athari walizopitia, walieleza masikitiko yao kwamba wamesahaulika huku wanasiasa wakiendelea kueneza hali inayoweza kurejelea matukio ya miaka iliyopita.
Kulingana na Bi Linah Mboasi, ambaye ni mmoja wao, wana wasiwasi wakati uchaguzi mkuu wa mwaka huu unakaribia.
“Tunaona wanasiasa wakitupiana maneno. Tafadhali, hatuwezi kuwa wahanga wa kila kipindi cha uchaguzi kisha tukaachwa tukihangaika wenyewe. Tumekuwa tukipiga kura na bado tunatarajia kupiga kura ifikapo mwezi wa Agosti, mwaka huu. Lakini kwa matatizo tunayokumbana nayo, je kama Wakenya tumesahaulika?” akasema Bi Mboasi.
Mratibu wa kikundi cha wakimbizi kanda ya Pwani, Bw Eliath Mbuuta, alisema serikali ilikuwa imewaahidi fidia laki – ni wengi wao hawajapokea chochote tangu walipoathirika kuanzia uchaguzi wa mwaka wa 2007.
Alieleza kuwa, baadhi ya waathiriwa walifariki kabla kulipwa fidia na imekuwa vigumu jamaa zao kufuatilia malipo hayo hata wakiwa na hati zote zinazotakikana.
“Hivi majuzi tulikuwa Nakuru mkutanoni lakini hakuna hatua zimepigwa. Kuna ada ambayo kufikia sasa bado hatujui ni nani anayepaswa kutufidia,” akasema.
Bw Mbuuta aliwataka viongozi kufanya kampeni za amani kuelekea kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Bi Emma Njeri, ambaye ni mmoja wa waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi alisema aliathirika na ghasia za uchaguzi katika chaguzi kuu tatu zilizopita.
Huku ikisalia takriban miezi mitano kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti, ana wasiwasi kuhusu usalama wake na wa familia yake.
“Mwaka wa 2007, wavulana wenye umri usiozidi miaka ishirini walikuja kwenye lango letu asubuhi wakiwa na mapanga na kututishia tupakie vitu na kuondoka. Tulipewa masaa kumi na mbili kutafuta sehemu nyingine. Hizo zilikuwa nyumba za kupangisha tulikuwa tunaishi,” asema Bi Njeri.
Karibu saa kumi na mbili jio – ni siku hiyo, anasema kikundi cha vijana kilirudi na kuanza kuwapiga watu, kuiba vifaa vyao vya nyumbani na hata kuwaua wengine kwa mapanga.
“Niliondoka kanisani peke yangu, ilinibidi niwaache wato – to wangu kwa sababu sikuwa na uhakika kama ni salama. Nilikuta nyumba yangu imevunjwa na kila kitu kimeibiwa ikiwa ni pamoja na godoro. Jirani yangu ambaye alikuwa amefumbia macho vitisho hivyo alikatwakatwa,” asema Bi Njeri huku akilia.
Bi Njeri anasema walijaribu mara kwa mara kuomba serikali iwalipe fidia walizoahidiwa laki – ni bado hawajafanikiwa.
“Imekuwa zaidi ya miongo miwili na bado nafuatilia fidia. Ni – na wajukuu wanaonitegemea. Mimi ni mgonjwa na sina pesa za kununua dawa. Serikali imetusahau,” asema Bi Njeri.
Mwenzake, Bw Kiletu Maingi, 62, anasema hadi leo miguu yake bado ina maumivu. “Nilipigwa vibaya sana huku mikono yangu ikiwa imefungwa mgongoni. Vijana hao walikuwa wakorofi,” alisema.
Next article
Jubilee sasa mbioni kukabili UDA Bonde la Ufa