Wafanyikazi shambani kwa Ruto wagoma
NA LUCY MKANYIKA
ZAIDI ya wafanyikazi 100 wa shamba linalohusishwa na Naibu Rais William Ruto waligoma kulalamikia kutolipwa mishahara yao.
Jana asubuhi, wafanyikazi hao waliandamana katika afisi ya sham – ba hilo ili kudai mishahara yao ya wiki sita.
Baadhi ya wafanyikazi ambao ni vibarua katika shamba hilo la Kisima, walisema kuwa juhudi za kutaka wasimamizi wao kuwalipa hazijafua dafu.
Walidai kuwa wamekuwa wakipokea vitisho kutoka kwa wasimamizi hao wanapodai mishahara yao.
Mmoja wa wafanyikazi hao, Bw Fred Mashauri alisema kuwa msimamizi wa shamba hilo Bw Arie Dempers, aliwaahidi kuwalipa mshahara wa siku mbili licha ya wao kudai wiki sita.
“Sisi tunataka mishahara yetu. Hatutarudi kazini hadi pale watakapotulipa pesa zetu zote. Gharama ya maisha imepanda mno na tunadaiwa kila pembe sababu hatulipwi mishahara yetu,” akasema.
Alidai kuwa licha ya kufanya kazi shambani humo kwa miaka tano, bado angali akifanya kazi kama kibarua.
“Wengi wetu ni vibarua na hakuna hatua yeyote inayochukuliwa ili tuajiriwe. Mshahara wenyewe ni duni,” akasema.
Vilevile, Bw Alex Saidi alisema kuwa wafanyikazi hao watasalia nyumbani hadi pale watakapopata mishahara yao.
“Tuna ushuhuda kuwa kila siku biashara inafanywa vizuri hapa. Hatuelewi kwa nini wasimamizi hawa hawataki kutulipa mishahara yetu,” akasema.
Juhudi za kutafuta meneja wa shamba hilo Bw Dempers ziliambulia patupu kwani hakuchukua simu na kujibu jumbe zetu.
Shamba hilo lililoko karibu na ziwa la Jipe lilinunuliwa na Naibu Rais kutoka kwa aliyekuwa mbunge wa Taveta Bw Basil Criticos.
Meneja huyo husimamia ukulima wa mahindi na ufugaji wa ng’ombe za nyama.
Mnamo 2019, Bw Dempers alikamatwa baada ya kutishia waumini wa msikiti mmoja katika eneo hilo waliokuwa wakiswali maombi ya alfajiri.
Vilevile, mnamo 2020 alijipata pabaya baada ya serikali ya kaunti ya Taita Taveta kudai kuwa alikuwa amefungia bomba la maji na kusababisha mamia ya wenyeji wa eneo hilo kukaa kiu.
Next article
KPA yashtakiwa kuhusu zabuni ya ujenzi bandari