Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa walia bei ya juu ya chakula cha mifugo
NA LAWRENCE ONGARO
WAFUGAJI wa ng’ombe wa maziwa wa Gatundu Kaskazini, wanaendelea kuhesabu hasara kutokana na kupanda kwa bei ya chakula cha mifugo.
Wafugaji hao wanadai kuwa mifugo yao haipati chakula kinachostahili huku utoaji wa maziwa ukiwa wa hali ya chini.
Bi Jane Nyokabi ambaye ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa katika kijiji cha Mitero, anasema wamelazimika kulisha mifugo yao nyasi, mabaki ya chakula cha kuku, na matawi ya ndizi.
Anasema bei ya juu ya chakula cha mifugo imesababisha wafugaji wengi kurejelea ufugaji wa kawaida wa kuwapa mifugo chochote kinachostahili kuliwa ili angalau wapate maziwa.
Bi Nyokabi alisema tangu mwaka 2021, wafugaji wa ng’ombe wa maziwa wamepitia masaibu mengi huku mifugo yao ikitoa kiasi kichache cha maziwa kwa kukosa chakula kinachofaa.
Wafugaji hao wanapendekeza serikali kuingilia kati na kupunguza bei ya chakula cha mifugo, ili wafugaji wengi wanufaike na ufugaji huo.
“Siku hizi ng’ombe wengi wanatoa maziwa kidogo ikilinganishwa na hapo awali kutokana na kukosa chakula kinachostahili,” alifafanua Bi Nyokabi.
Anasema gunia moja la chakula cha ng’ombe hapo awali liliuzwa kwa Sh2,000 lakini sasa bei imeongezeka hadi Sh3,000.
Anazidi kueleza kuwa hata viwanda vingi vya maziwa vimekosa kupata maziwa ya kutosha kutokana na hali hiyo.
Kulingana na wakulima hao hata uzito wa mifugo umepungua kwa kiwango kikubwa.
Naye Bw Joseph Kahonge alisema kuwa wafugaji wengi wamebaki kutafuta chakula cha ng’ombe kwa kutafuta chochote kile kinachoweza kuwafaa.
Anapendekeza serikali kupunguza ushuru wa kuingiza chakula cha mifugo hapa nchini ili mfugaji wa kawaida aweze pia kunufaika.
Anaeleza kuwa wengi wa wafugaji wanategemea kazi hiyo kujikimu kimaisha ili kupeleka watoto shuleni.
“Tunaiomba serikali kuingilia kati jambo hilo ili wafugaji waweze kupata afueni ya kulisha mifugo bila matatizo,” akasema Bw Kahonge.
Alieleza kuwa wakati kama huu mvua inanyesha wafugaji wana kibarua kikubwa kufanya juhudi ya kutafutia mifugo chakula.
Next article
Tim Wanyonyi hatimaye atangaza kuunga mkono Igathe kwa kiti…