HATIMAYE wahudumu katika sekta ya uchukuzi Kaunti ya Murang’a wameanza kupata afueni baada ya kampuni za usambazaji petroli na dizeli kumakinikia ukosefu ambao ulikuwa umedumu kwa siku sita kufikia jana Ijumaa.
Uhaba huo ulikuwa umezuka baada ya serikali kuzozana na wasambazaji mafuta nchini kuhusu kitita ambacho wanafaa kupata cha kuwafanya wapunguzie Wakenya bei ya mafuta.
Kitita hicho hukusanywa kutoka kwa ushuru ambao wateja wa mafuta hutoa. Kwa sasa kitita hicho ni Sh5.44 kwa lita moja na ambacho hatimaye hurejeshewa wasambazaji hao wa mafuta kama mbinu ya kuziba pengo la hasara baada ya kuuza kwa bei iliyopigwa shoka.
Serikali ilituhumiwa kwa kugawa kitita hicho ambacho kilijumlishwa kuwa Sh39 bilioni kwa njia za kutomakinikia haki na kama njia ya kushinikiza uadilifu katika mgao huo, wasambazaji hao wakasusia kufikisha mafuta mashinani hivyo basi kusababisha uhaba.
Hali hiyo ilizua kilio na presha ikaelekezwa kwa serikali hadi ikalipa.
Kwa sasa, kuna foleni ndefu katika vituo vya mafuta huku wahudumu wa bodaboda, magari, tuktuk na walio na mitambo ya jenereta wakijitokeza kwa wingi huku wengine wakibebana na vibuyu na mitungi ili wajipe hata ya ziada.
“Kwa sasa hali imeimarika na uhaba ambao ulikuwa umelemaza shughuli za uchukuzi na pia usagaji wa bidhaa kama unga na chakula cha mifugo kwa sasa umetokomaa. Kile sasa tunapambana nacho ni foleni ndefu lakini tumehakikishiwa kwamba hali itarejea kuwa ya kawaida kabla ya jua la Jumapili kutua,” akasema Kamishna wa Kauti Bw Karuku Ngumo.
Bw Ngumo alionya wenyeji dhidi ya kuhifadhi petroli katika nyumba zao za makazi akitaja hatua hiyo kama hatari kwa maisha na mali.
“Mvuke wa petroli ni hatari sana na huenda aliye na mbinu ya kuihifadhi katika nyumba yake ajipate pabaya sana. Moto ukizuka, tutapoteza uhai na mali na hatutaki kukwamuka kutoka tatizo la ukosefu wa mafuta haya kisha tuingie kukuomboleza wewe tukikupangia mazishi,” akasema.
Kwa kuhofia kwamba huenda ukosefu huo urejelee uchumi wa taifa, wengi wa watumizi wanajinunulia hata ya ziada na kuyahifadhi kwa mitungi na vibuyu katika maboma yao.
“Hakuna haja ya kuhatarisha maisha yako na ya wengine pia ukisaka kujipa afueni. Acha mafuta yakae tu kwa vituo vya petroli. Hata yakiadimika tena, sio eti ni wewe peke yako utaathirika. Tutaathirika sote. Nawaomba tukome huo mtindo. Huwezi kwa mfano, ukakimbia hospitalini ukiwa mgonjwa, na ukishapata dawa unaagiza za ziada eti za kujikinga katika siku za usoni. Tukosoane tu na tusemezane ukweli kwamba hakuna haja ya kununua petroli kwa mitungi na unaenda kuificha kwa mvungu wa kitanda chako. Utaungua,” akasema.
Lori hili laonekana ndilo suluhu ya uhaba wa mafuta linapoingia mjini Murang’a likiwa tani 27 za petroli Ijumaa, Aprili 8, 2022 katika kituo cha Kenol. PICHA | MWANGI MUIRURI
Hayo yanajiri huku Waziri wa Kawi nchini Bi Monica Juma akiwahakikishia Wakenya kwamba kuna mafuta ya kutosha na changamoto iliyokuwa imezua uhaba huo wa wiki moja imekabiliwa.
“Ningetaka Wakenya wajue kwamba katika vituo vyetu vya mafuta kwa sasa hakuna uhaba. Pia, ningetaka kuwahakikishia kuwa mabomba yetu yamejaa pomoni. La tatu, meli za kuleta mafuta nchini ziko baharini zikija kama ilivyoratibiwa. Watu waache kuwa na wasiwasi kwa kuwa hali iko thabiti,” akasema.
Bi Juma alisema kwamba kwa sasa kile angewaomba Wakenya ni wakome mtindo wa kupiga foleni “kwa kuwa baadhi ya wafanyabiashara hao wa vituo vya mafuta wanaweza wakaingiwa na ulafi wa kuunda vya haramu.”
Alisema huenda wengine waongeze bei au wayachanganye mafuta na maji wakiona wateja wamezidi bidhaa waliyo nayo katika mapipa yao ili vipimo vya ziada viwe faida ya bwerere.
“Tuwe na utaratibu wa kawaida wa kufika katika vituo vya mafuta na tujipe huduma kwa upole bila ya kufinyana au kung’ang’ania na hali itathibitika katika muda wa siku mbili zijazo,” akasema waziri Juma.