Connect with us

General News

Wakazi waisifia serikali kwa kumwaga mamilioni kupanua daraja – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wakazi waisifia serikali kwa kumwaga mamilioni kupanua daraja – Taifa Leo

Wakazi waisifia serikali kwa kumwaga mamilioni kupanua daraja

NA KALUME KAZUNGU

WAKAZI wa Kaunti ya Lamu wameisifia serikali ya kaunti hiyo kwa kutenga mamilioni ya pesa kuanzisha upanuzi na ujenzi wa daraja la kisiwa cha Faza.

Wakizungumza na Taifa Leo, wakazi hao walisema mpango huo utakaogharimu Sh19 milioni utawaondolea utovu wa usalama na kuyapa magari, pikipiki na punda nafasi ya kutosha ya kusafirisha bidhaa.

Bw Khaldun Vae, mkazi, alisema mbali na wakazi wa kisiwa cha Faza, upanuzi wa daraja hilo pia utawanufaisha wananchi wa visiwa jirani, vikiwemo Mtangawanda, Mbwajumwali, Tchundwa, Kizingitini, Myabogi, Siyu, Bori, Shanga, Bahamisi na Pate.

“Tunafurahia kupanuliwa kwa kivuko chetu. Hiyo inamaanisha usafiri pia utakuwa salama na wa haraka kinyume na awali ambapo daraja hili halingeruhusu magari, punda na wenye miguu kuvuka kwa wakati mmoja,” akasema Bw Vae.

Bi Fatma Ali naye alisema kutokana na hatari iliyokuwa imewakodolea macho, walilazimika kubandika jina daraja hilo na kuliita ‘Daraja la Mauti.’

“Tumeomba kwa muda mrefu daraja letu likarabatiwe na kupanuliwa. Nashukuru kwamba serikali hatimaye imesikia kilio chetu na imechukua hatua ya kukarabati daraja letu la mauti,” akasema Bi Ali.

Mwaka jana, abiria aliyekuwa akisafirishwa kwa pikipiki alifariki papo hapo huku dereva wa pikipiki hiyo na mwenye punda wakijeruhiwa vibaya pale pikipiki ilipogongana na punda huyo kwenye kivuko hicho kabla ya kutumbukia baharini.

Hapo 2016, maafisa saba wa polisi na raia wawili walijeruhiwa vibaya pale gari walimokuwa wakisafiria ilipokosa mwelekeo na kutumbukia baharini wakati ikiendeshwa kwenye daraja hilo.

Daraja la Faza linalopanuliwa kwa kima cha Sh19 milioni. PICHA/ KALUME KAZUNGU

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa kivuko hicho, gavana wa Lamu, Fahim Twaha alisema mradi huo utachukua miezi minne kukamilika.

Kivuko hicho ni kiunganishi cha kipekee kwa wale wanaoingia na kutoka mjini Faza na hutegemewa na wakazi karibu 3,000.

Kwa miaka mingi, kivuko hicho kimechangia ajali na hata maafa kwa watumiaji kutokana na wembamba wake.

Daraja hilo lina urefu wa mita 500 na upana wa mita 2.5 pekee, hali ambayo imekuwa ikizuia watumiaji, ikiwemo wanaotembea kwa miguu, punda, baiskeli, pikipiki na magari.

Bw Twaha alisema ujenzi uliozinduliwa unalenga kulipanua daraja hilo kwa mita 2.5 zaidi ili kufikia upana wa angalau mita tano.

Pia itajengewa reli upande wa kandokando ili kudhibiti zaidi usalama wa wanaovuka kwenye daraja hilo.

“Tumeamua kuanzisha upanuzi wa daraja hili ili kuzuia ajali za watu, punda, magari na baiskeli kuanguka ndani ya bahari wanaposafiri. Upanuzi pia utasaidia kupunguza muda unaotumika wakati watu, punda na magari yanapolazimika kusubiri ili kupishana kutumika kivuko hicho,” akasema Bw Twaha.