Wakenya 3.5m hatarini kufa njaa ukame ukizidi
NA COLLINS OMULO
WAKENYA 3.5 milioni wanakabiliwa na hatari ya kukosa chakula kutokana na ukosefu wa mvua ya kutosha, Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Ukame (NDMA) imesema.
Haya yanajiri huku Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya (KMD) ikionya kwamba mzozo wa sasa utakuwa mbaya zaidi kwa kuwa mvua haitanyesha karibuni.
Idara hiyo ilisema kwamba hali ya sasa ya ukame inayoshuhudiwa katika maeneo kame inatarajiwa kuendelea huku maeneo mengi ya nchi yakitarajiwa kuwa na kiangazi kwa miezi mitatu ijayo.
Hali hii mpya inajiri wakati ambao juhudi za serikali za kukabiliana na mzozo huo zikiwa hafifu huku ikiangazia uchaguzi mkuu wa Agosti 9.Maeneo kame ni asilimia 89 ya nchi na yanaishi asilimia 36 ya raia wa Kenya.
Kinaya ni kuwa Sh44 bilioni zimetengwa kwa uchaguzi mkuu na hata uchaguzi wa duru ya pili.
Kulingana na ripoti ya kila mwezi ya hali ya ukame nchini ya NDMA, kiangazi kikali kinaendelea katika kaunti 17 kati ya 23 kame kote nchini Kaskazini, Kaskazini Mashariki na maeneo ya Pwani kwa misimu mitatu iliyofuatana.
Hii imefanya idadi ya watu wanaohitaji msaada wa kibinadamu kuongezeka kutoka 3.1 milioni mwezi wa Februari hadi 3.5 milioni kwa wakati huu, huku ripoti ikiomba serikali kuongeza msaada wa chakula na pesa zinazotumiwa familia zinazokumbwa na njaa.
Kaunti nane za Marsabit, Mandera, Wajir, Samburu, Isiolo, Baringo, Turkana na Laikipia ziko katika hatari zaidi ya ukame huku hali ikiendelea kudorora katika kaunti za Isiolo, Laikipia na Samburu.
NDMA inasema kuwa kaunti za Garissa, Kilifi, Kitui, Kwale, Tana River, Lamu, Meru (Kaskazini), Nyeri (Kieni) na Pokot Magharibi ziko katika hatari ya kukumbwa na ukame.
Kaunti zilizobaki za Kajiado, Narok, Makueni, Taita Taveta, na Embu (Mbeere) ziko katika hali ya kawaida ya kiangazi huku Tharaka Nithi ikiwa katika hali ya kuondoka kutoka ukame.
“Hali hii imesababishwa na ukosefu wa mvua ya kutosha mwaka wa 2021 kuongezea kukosa mvua katika misimu miwili iliyotangulia na kuchelewa kwa mvua mwaka wa 2022,” inasema ripoti ya NDMA.
Mwaka 2021, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza ukame unaoendelea kuwa janga la kitaifa na akaagiza Wizara ya Fedha na Usalama wa Ndani kuongoza juhudi za serikali za kusaidia waliothiriwa na maji na kuwapa chakula cha msaada pamoja na kununua mifugo kuepuka vifo.
Kulingana na utabiri wa Idara ya utabiri wa hali ya hewa, hali ya sasa ya uhaba wa maji, chakula na lishe kwa binadamu na wanyama katika maeneo kame inatarajiwa kuwa mbaya zaidi.