Wakenya kuanza kuvaa maski tena kuzuia Covid-19
MARY WANGARI NA HELLEN SHIKANDA
SERIKALI sasa inawataka Wakenya kuanza tena kuvaa maski huku wasiwasi ukitanda kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa wimbi jipya la maambukizi ya Covid-19.
Wizara ya Afya imesema kuwa idadi ya maambukizi kwa sasa imefikia asilimia 5.6 huku jumla ya asilimia 3.3 ikirekodiwa kila wiki ambapo visa vimekuwa vikipanda tangu mwanzoni mwa Mei.
“Tunawahimiza Wakenya kuvaa maski zao. Tunahofia kuwa visa vya Covid-19 vinaongezeka,” alisema Mkurugenzi wa Afya ya Umma katika Wizara ya Afya, Dkt Francis Kuria.
“Tulipositisha baadhi ya masharti ya kudhibiti Covid-19, kiwango cha maambukizi kilikuwa karibu asilimia 1. Kufikia mwanzoni mwa Mei, kilikuwa karibu asilimia 0.1 lakini ghafla, tuna jumla ya asilimia 3.3 kwa wiki na kiasi cha juu zaidi cha asilimia 5.6,” alifafanua.
Haya yamejiri siku chache tu baada ya Wizara ya Afya mnamo Jumapili, kurekodi visa 128 na asilimia 5.6 ya kiwango cha maambukizi ambacho ni cha juu zaidi katika muda wa miezi minne iliyopita.
Watu 128 walipatikana na virusi vya corona miongoni mwa vipimo 2,303 vilivyochukuliwa katika muda wa saa 24 na kufanya jumla ya idadi ya visa vilivyothibitishwa kufikia 324,686; ilisema taarifa kutoka kwa Wizara ya Afya.
Kufikia Jumapili, Kaunti ya Nyeri ilikuwa inaongoza kwa idadi ya maambukizi ikirekodi visa 68, na kufuatiwa na Nairobi (54), Kiambu na Kisumu visa viwili kila moja huku Kakamega na Siaya zikirekodi kisa kimoja kila moja, kulingana na takwimu hizo.
Hata hivyo, hakuna kifo kilichorekodiwa kutokana na virusi hivyo.
Tangu kuzuka kwa janga hilo la kimataifa, Kenya imepoteza watu 5,651.
Wataalam wa afya, hata hivyo, wamesema huenda Kenya ikakosa kurekodi idadi kubwa ya visa na kuenea kwa maambukizi baina ya wanajamii jinsi ilivyoshuhudiwa katika mikurupuko ya awali.
“Tunaweza kuwa na uhakika kwamba hatutaona idadi kubwa ya wagonjwa wanaolazwa hospitalini na vifo kwa sababu watu wanaokabiliwa na hatari zaidi wamepokea chanjo na tuna kinga ya kijamii kutokana na maambukizi ya awali,” alieleza Dkt Ahmed Kalebi, mtaalam kuhusu maambukizi ya virusi.
Dkt Kalebi alifafanua kuwa idadi ya visa hivyo si ya kuhofisha mno kwa sababu huenda ndiyo kiwango cha juu zaidi kitakachoshuhudiwa cha maambukizi ya gonjwa hilo katika msimu huu wa maradhi ya mafua yanayotarajiwa kufikia kilele mwishoni mwa mwezi.
“Hatutaona takwimu zikipanda sana lakini hilo halimaanishi tusiwe makini. Tunapaswa kuzingatia mikakati ya kujikinga na kuvaa maski zetu ili kuwa salama,” alishauri.
Kiwango cha maambukizi ya virusi vya corona kinapanda wakati huu ambapo ni idadi ndogo tu ya Wakenya wanaoendea chanjo huku wasafiri wakiwa ndio pekee wanatafuta chanjo.
Kufikia wiki jana, ni asilimia 31 pekee ya watu wazima waliokuwa wamepokea chanjo kamili huku dozi 4,712 za chanjo zikitolewa Jumamosi.