Uvamizi: Wakenya watakiwa waondoke Ukraine haraka iwezekanavyo
NA MARY WANGARI
WAKENYA wanaoishi katika taifa la Ukraine lililogubikwa na mashambulizi makali kutoka kwa Urusi, wametakiwa “kuhama kwa dharura” au “kumakinika zaidi.”
Ubalozi wa Kenya jijini Vienna, Austria, unaokaribia Ukraine, ulitoa taarifa Ijumaa, Februari 25, ukiwashauri raia wake kuhamia kwingineko hadi watakaposhauriwa vinginevyo.
“Kufuatia taharuki inayozidi kuongezeka pamoja na mashambulizi makali yaliyotekelezwa katika eneo la Ukraine na taifa la Urusi mnamo Februari 24, Wakenya wote wanaoishi au kusomea Ukraine wanashauriwa kuondoka Ukraine na kukaa mbali hadi ilani nyingine itakapotolewa,”
“Wanaotaka kuendelea kuishi humo wanashauriwa kuwa makini zaidi,” ilisema taarifa hiyo kutoka kwa Ubalozi wa Kenya nchini Austria.
Aidha, Ubalozi huo umewataka raia wa Kenya waliomo Ukraine kuwasiliana nao kupitia simu nambari: +4317123919 au baruameme [email protected], [email protected], kwa hali yoyote ua dharura.
Wanaweza pia kuwasiliana na Ubalozi wa Kenya nchini Ukraine kupitia nambari: +38 (044) 229 79 13 au baruameme [email protected].
Wakati huo vilevile kundi la wanafuni Wakenya wanaosomea Ukraine wameiomba usaidizi wa kuondoka Ukraine mashambulizi kutoka kwa vikosi vya Urusi yakishika kasi na kuzua taharuki kote nchini Ukraine.
Wanafunzi hao waliozungumza na wanahabari walisema wanataka kuondoka Ukraine ila wanahitaji usaidizi kufanya hivyo.
“Umati wa watu wanaohama mijini lakini ni vigumu sana kusonga kwa sababu ya trafiki. Nafikiri tulitembea kwa kilomita saba. Kuna foleni ndefu nje ya duka za kuuzia dawa, ATM, watu kununua bidhaa kwa hofu na wasafiri kusongamana katika vituo vya treni ambavyo vimefutilia mbali baadhi ya safari,” alisema mwanafunzi kwa jina Asya kutoka jijini Kiev.
“Viwanja vya ndege vilifungwa hivyo basi hatuwezi kusafiri kwa ndege. Treni zilipandisha nauli kwa hivyo usafiri kutoka mji mmoja hadi mwingine ni ghali vilevile. Tunatakiwa kulipa Sh22,770 kwa safari tuliyokuwa tukilipa Sh5,692. Tunatumia vyeti vya wanafunzi na hatuna uwezo wa kutosha kujikimu,” alieleza Stephanie kutoka mjini Kharkiv.
Wanafunzi hao wametoa wito kwa Wizara ya Masuala ya Kigeni nchini Kenya kuwasaidia kupata vyeti vya dharura vya usafiri vitakavyowawezesha kuruhusiwa kuingia nchini Poland.
“Tunahitaji vyeti vya dharura vya usafiri kutuwezesha kuingia Poland kwa sababu kwa sasa viwanja vya ndege vimefungwa. Tutalazimika kuvuka mpaka na kisha kusafiri kwa ndege kutoka Poland,”
“Lakini kwa sababu tuna pasipoti za Kenya tunahitaji visa ya kuingia Poland ambayo hatuwezi kutuma ombi kwa sasa. Kisha tukifika hapoi, si kila mtu ataweza kulipia nauli ya ndege kwa sababu wengine hawakuwa wamepangia tukio hili,” alihoji Asya.
“Kwa walio na pesa huenda wasiweze kuzipata kutokana na foleni ndefu kwenye ATM hauna hakika utafikiwa na ukifaulu hauna hakika pesa zitakuwepo, ikiwa kuna hela kuna kiwango cha pesa unachoweza kutoa,”
“Iwapo ulikuwa utumiwe pesa kupitia Western Union, zimefungwa hivyo basi hata kama una pesa hungeweza kuzipata,” alisema mwanafunzi huyo.
Next article
ZARAA: Trei ni muhimu kwa kilimo cha mahindi hasa katika…