Connect with us

General News

Wanasheria washauri wabunge waondoe makali ya kuumiza raia katika Mswada wa Fedha, 2022 – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wanasheria washauri wabunge waondoe makali ya kuumiza raia katika Mswada wa Fedha, 2022 – Taifa Leo

Wanasheria washauri wabunge waondoe makali ya kuumiza raia katika Mswada wa Fedha, 2022

NA CHARLES WASONGA

WABUNGE wametakiwa kuufanyia marekebisho Mswada wa Fedha unaopendekeza kujumuishwa kwa unga wa mahindi na ngano katika orodha ya bidhaa zinazotozwa ushuru wa thamani ya ziada (VAT).

Kwenye memoranda iliyowasilishwa kwa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha inayokusanya maoni kutoka kwa umma kuhusu mswada huo, Chama cha Mawakili Nchini (LSK), kimelalamika kwamba kutozwa VAT bidhaa hizo kutawaathiri Wakenya zaidi.

“Tayari bei ya unga wa mahindi imepanda hadi kufika Sh150 kwa paketi moja ya kilo mbili jijini Nairobi huku unga wa ngano ukiuzwa kwa Sh170 . Bila shaka bidhaa hizi zikitozwa VAT ya kima cha asilimia 16 bei itapanda zaidi, hali itakayowaumiza wananchi wenye mapato ya chini,” ikasema memoranda hiyo iliyotiwa saini na rais wa LSK Eric Theuri.

“Hii ndio maana tunawataka wanachama wa kamati hii na wabunge wote kuondoa sehemu ya mswada huu inayopendekeza unga wa mahindi na ngano kutozwa VAT,” memoranda hiyo ikaongeza.

Mswada huo wa Fedha wa 2022 uliowasilishwa bunge mnamo Aprili 11, 2022 unalenga kuiwezesha serikali kukusanya jumla ya Sh50.53 bilioni kwa ajili ya kufadhili bajeti ya Sh3.3 trilioni ya mwaka wa kifedha wa 2022/2023.

LSK ilisema ingawa serikali imejitolea kuimarisha mapato yake, haifai kutumia hali hiyo kama kisingio cha kutoza ushuru bidhaa za kimsingi.

Chama hicho cha wanasheria nchini ni miongoni mwa mashirika 58 ambayo yalialikwa kutoa maoni na mapendekezo yao kuhusu mswada huo katika vikao vyake vya umma.

LSK pia inakosoa sehemu zingine 22 katika mswada huo ambazo inasema zinaharibu mazingira ya kufanyia biashara na kuanzisha viwanda nchini.

Bw Theuri anasema kuwa ikiwa wabunge wataupitisha mswada huo bila kuufanyia marekebisho kwa kuondoa sehemu zinazoongeza ushuru kwa bidhaa za kimsingi, LSK itawasilisha kesi kortini kuupinga.

“Mswada ambao unawaongeza wanachini gharama ya maisha ni mbovu na unakwenda kinyume na Katiba. Mswada kama huo pia unaweza kuleta misukosuko na hali ya utovu wa usalama nchini,” LSK inasema.

Kando na kutoza VAT kwa unga wa mahindi na ngano, mswada huo pia unapania kuongeza ushuru unaotozwa pikipiki, vipodozi na bidhaa za urembo, vipuli, pombe, mvinyo, chokoleti na maji ya chupa.

Ushuru unaotozwa pikipiki zinazoagizwa kutoka nje utaongezwa kuwa Sh13,403.64 kila moja kutoka Sh12,185.16, ushuru wa pombe utaongezwa kwa kima cha asilimia 10, mvinyo (asilimia 20), matangazo ya pombe (asilimia 15), vipodozi na bidhaa za urembo (asilimia 15).

Mawakili hao pia walitoa wito kwa Wakenya kuwatia presha wabunge waondoe sehemu za mswada huo zinazopendekeza kuongezwa kwa gharama ya maisha.

Kando na bidhaa za kimsingi, mswada huo pia unapendekeza kuongezwa kwa ushuru kwa nguo na vifaa vya kimatibabu, hali ambayo itaongeza gharama ya matibabu.

Hii walisema inakwenda kinyume na sera ya serikali kuu ya kupunguza gharama ya matibabu.

LSK pia inasema kuwa mswada huo unachangia bidhaa zinazotengenezwa nchini kuwa ghali kwa kuongeza ushuru unaotozwa viwanda.

“Hii ina maana kuwa taifa hili litalazimika kuagiza bidhaa ambazo zinaweza kutengenezwa nchini. Uagizaji wa bidhaa hizo pia ni ghali kutokana na kudorora kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni, haswa dola ya Amerika,” inasema memoranda hiyo ya LSK.

Kamati hiyo ya Fedha, inayoongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Homa Bay itakusanya maoni na mapendekezo, kuhusu mswada huo, kutoka kwa umma hadi Ijumaa, Mei 13, 2022.

Baadaye itawasilisha ripoti yake kwa kikao cha bunge lote wiki ijayo kwa wabunge kujadili mapendekezo yao ili kuvusha mswada huo katika hatua ya pili ya kushughulikiwa na wabunge.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending