Connect with us

General News

Wanasiasa waombea shida walizochangia kuwaletea Wakenya – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Wanasiasa waombea shida walizochangia kuwaletea Wakenya – Taifa Leo

Wanasiasa waombea shida walizochangia kuwaletea Wakenya

NA LEONARD ONYANGO

VIONGOZI wa kisiasa wamekongamana leo Alhamisi katika hoteli ya Safari Park kwa kiamsha kinywa kuombea nchi huku mamilioni ya Wakenya wakihangaishwa na baa la njaa na gharama ya juu ya maisha.

Maombi hayo ya kila mwaka huandaliwa na Bunge, ambapo viongozi wanaohudhuria huombea changamoto mbalimbali zinazokumba nchi.

Miongoni mwa changamoto zinazokumba Wakenya ni bei ya juu ya bidhaa, baa la njaa na ukosefu wa usalama.

Wakenya milioni 3.3 kote nchini wanakabiliwa na makali ya njaa lakini wanasiasa, ambao wengi wao wanahudhuria mkutano wa leo Alhamisi, wanaonekana kutojali.

Wakulima wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa mbolea katika msimu huu wa upanzi lakini wabunge na viongozi wengine wa kisiasa wamezama kwenye kampeni.

Wabunge hao hao wameanza juhudi za kutaka kuwaongezea Wakenya mzigo mzito zaidi kwa kudai nyongeza ya mishahara kwa asilimia 62.

Iwapo Tume ya Kutathmini Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC) itakubali maombi yao, kila mbunge wa Bunge la 13 atalipwa Sh1.15 milioni kwa mwezi kutoka Sh 621,250 ambazo wanalipwa sasa.

Wabunge pia wamepinga vikali pendekezo la SRC la kutaka marupurupu ya Sh5,000 ambayo kila mbunge hulipwa anapohudhuria vikao Bungeni yafutiliwe mbali.

Wakosoaji wanasema kuwa ni kinaya kwa viongozi hao wa kisiasa kuombea Wakenya ilhali wanachangia kwa kiasi kikubwa changamoto zinazokumba nchi.

Kulingana na kamati andalizi, ratiba ya leo imeachiwa viongozi wa kidini katika juhudi za kuzima cheche za siasa.

Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake William Ruto na kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga wanatarajiwa kuhudhuria ibada hiyo ya 19 ya kuombea taifa.

Kulingana na mwenyekiti wa kamati andalizi, mbunge wa Makueni Dan Maanzo, siasa haitaruhusiwa katika ibada hii ya leo.

Alisema kuwa Bunge pia limealika wageni kutoka Uganda, Tanzania na Congo.

Iwapo wanasiasa wataruhusiwa kuhutubu, itakuwa vigumu kuwazuia kurushiana cheche za maneno haswa ikizingatiwa kuwa zimesalia siku 72 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti.

Mwaka 2021, maombi hayo yalifanyika katika majengo ya Bunge ambapo watu wachache walioalikwa walihudhuria.

Wakili Peter Waiyaki alikuwa mgeni rasmi aliyehutubia waliohudhuria akiwemo Rais Kenyatta.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Trending