Wandani wa Ruto sasa wanadai sheria ya vyama itawafaa, huenda wasiipinge kortini
Na CHARLES WASONGA
HUENDA wandani wa Naibu Rais William Ruto wasiwalishe kesi kortini kupinga utekelezaji wa sheria tata ya Vyama vya Kisiasa iliyotiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta Alhamisi, Januari 28, 2022.
Hii ni licha ya kwamba wabunge na maseneta wanaoegemea mrengo wa Tangatanga walipinga vikali kupitishwa kwa mswada wa sheria hiyo katika bunge la kitaifa na seneti katika vikao vilivyofanyika Desemba 2021 na Januari 2022.
Wandani hao wa Dkt Ruto sasa wanasema sheria hiyo, inayoruhusu kuundwa kwa vyama vya miungano, sasa itawafaa zaidi katika kurasimisha muungano wao mpya wa Kenya Kwanza.
Muungano huo unashirikisha vyama vya United Democratic Alliance (UDA), Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya.
Muungano huu ulibuniwa baada ya vinara wa vyama hivyo viwili, Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya) kujiondoa kutoka muungano wa One Kenya Alliance (OKA) na kutangaza kuwa watashirikiana na chama cha UDA kinachoongozwa na Dkt Ruto.
Wawili hao walichukua hatua hiyo katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi, Januari 23, 2022 wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) la ANC.
Washirika wa Dkt Ruto wanasema sheria hiyo mpya itatoa nafasi kwa wao kujenga muungano wa Kenya Kwanza ili kuboresha nafasi ya mgombea urais wa muungano huo kuibuka mshindi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.
Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja ambaye anaegemea chama cha ANC alisema Jumapili sheria hiyo itasaidia muungano huo sawa na itakavyosaidia wapinzani wao katika Azimio la Umoja.
“Ingawa mrengo wa Azimio ulidhani kuwa wao ndio wanahitaji zaidi sheria hiyo ya vyama vya kisiasa, tunahitaji sheria hiyo kwa sababu sisi pia tumeanza mchakato wa kubuni muungano kwa ajili ya kushinda katika uchaguzi mkuu ujao,” akawaambia wanahabari katika eneo la Ongata Rongai alipokuwa ameandamana na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi.
Mnamo Alhamisi wiki jana, Januari 28, 2022, baada ya mswada huo kupitishwa katika seneti, Bw Sakaja alirejelea kauli hiyo akiwaambia wenzao wa mrengo wa Azimio la Umoja wafahamu kuwa “hata sisi tutafaidika na mswada huu.”
“Yaliyomo katika sheria hii hayatatumika na mrengo mmoja pekee wakati wa uchaguzi. Yatatumika na pande zote. Ikiwa ni sheria mbaya itaathiri kila mtu. Ikiwa ni sheria nzuri, itafaidi kila mtu,” Bw Sakaja akaongeza.
Kwa upande wake Wakili Mkuu Ahmednassir Abdullahi alisema sheria hiyo pia itamsaidia Dkt Ruto kujenga muungano na viongozi wengine ili kuimarisha nafasi yake ya kushinda urais.
“Siasa ni mchezo wa ajabu. Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga walitumia rasilimali nyingi kuhakikisha kuwa mswada wa marekebisho ya sheria za vyama vya kisiasa umepita ili vinara wa OKA, Mudavadi, Kalonzo Musyoka na Wetang’ula wakubali kujiunga na Azimio la Umoja linaloongozwa na Raila na Dkt Ruto atengwe. Mswada ulipitishwa. Sasa Ruto ataitumia sheria kuwashirikisha wote ili kuboresha nafasi yake ya kuingia Ikulu,” wakili huyo akasema kupitia Twitter.
Kwa upande wake, seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen alisema, “Tumepitisha mswada wa marekebisho ya sheria za vyama. Bila shaka tumewapa Azimio kamba ambayo walitaka kutumia kujitia kitanzi. Mtu asije kwetu akilia baada ya mchujo utakaofanyika Aprili.”
Sawa na muungano wa Azimio la Umoja, sheria hiyo pia itawezesha vyama tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza – UDA, ANC na Ford-Kenya – kufaidi kutokana na pesa za hazina ya vyama vya kisiasa bila mitafaruku iliyoshuhudiwa katika muungano wa NASA uliosambaratika.
Mnamo Jumatano katika seneti, maseneta wa mrengo wa Azimio, waliwalemea wenzao wa mrengo wa Kenya Kwanza kwa kutupilia mbali hoja zote zao zote za marekebisho kwa mswada huo.
Kura ilipopogwa mrengo wa Azimio uliibuka washindi kwa kupata kura 28, kutaka mswada huo upitishwe bila kufanyiwa marekebisho yoyote huku ule wa Kenya Kwanza ukipata kura saba pekee.