[ad_1]
Wanyonyi asisitiza hataachia yeyote tiketi ya Azimio
Na WINNIE ONYANDO
MBUNGE wa Westlands, Tim Wanyonyi (pichani) ameshikilia kuwa hatakubali kumwachia yeyote tiketi ya muungano wa Azimio la Umoja katika kinyang’anyiro cha ugavana Nairobi.
“Niko tayari kupambana na yeyote atakayejitokeza kuwania kiti cha ugavana wa Nairobi kupitia tiketi ya ODM au muungano wa Azimio la Umoja. Sitajiondoa wala kumwachia nafasi mtu yeyote,” akasema alipokutana na kundi la wasomi kutoka eneo la Magharibi jijini Nairobi, Ijumaa.
“Wote waje tupimane kwenye debe kwa kuwa sina uwoga,” akasema Bw Wanyonyi aliyekuwa akizungumza jijini Nairobi alipokutana na kundi la wasomi kutoka eneo la Magharibi.
Kiongozi huyo ambaye amekuwa mbunge wa Westlands kwa mihula miwili alipuuzilia mbali madai kuwa mabwanyenye wa Mlima Kenya watamteua mtu wa kuwania kiti cha ugavana wa Nairobi kupitia tiketi ya muungano wa Azimio la Umoja unaoongozwa na Bw Raila Odinga.
“Niko tayari kabisa kuwania kiti hicho. Hata chama changu cha ODM kinajua kuwa ni mimi pekee ndiye nimejitokeza kuwania kiti hicho. Ikiwa watampendekeza mwingine, basi tukutane naye debeni,” akasema Bw Wanyonyi.
Alieleza kuwa nia yake ya kuwania kiti cha ugavana ni kuleta maendeleo kama kiongozi na si kama mwanasiasa.
Baadhi ya viongozi wengine ambao wametajwa au kutangaza nia ya kuwania ugavana ni Johnson Sakaja ambaye hajatangaza chama atakachotumia kuwania kiti hicho, mfanyibiashara Ann Kagure, mhubiri Margaret Wanjiru (UDA) na Richard Ngatia anayepigiwa upatu kwamba huenda akapeperusha bendera ya Azimio la Umoja.
[ad_2]
Source link